Matumaini yarejea katika mahusiano ya Marekani na China
20 Juni 2023Wakati akikamilisha ziara yake nchini China, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alikutana kwa mazungumzo na Rais wa China Xi Jinping, na wawili hao wamekubaliana kurejesha mahusiano mema kati ya mataifa hayo, ambayo kwa muda sasa yamekuwa yakidorora.
Hata hivyo Blinken ameondoka Beijing huku ombi lake kuu la kutaka kurejesha mawasiliano ya kijeshi likikataliwa na China. Marekani inayapa umuhimu mahusiano hayo ya kijeshi ili kuepuka migogoro hususan kuhusu Taiwan.
Marekani na China pia zimeshindwa kufikia makubaliano kuhusu masuala kadhaa huku kila upande ukionekana kusalia na msimamo wake hasa kuhusu masuala ya kibiashara, mzozo wa Taiwan, haki za Binaadamu huko China na Hong Kong na hata uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Soma pia: Biden asema mahusiano na China yanafuata "mkondo sahihi"
Blinken amesema aliibua wasiwasi wake kuhusu namna China inavyowatendea watu wa jamii ya wachache wa Uyghur na Tibet wa huko Hong Kong, ambako Beijing imezuia vikali uhuru wa kujieleza. Blinken aliyazungumza hayo hadharani baada ya kukutana na maafisa wa China, ambao huchukulia vibaya ukosoaji kuhusu haki za binadamu, hasa unapokuwa katika ardhi yao.
China na Marekani kuwa na uhusiano thabiti
Blinken na Xi wote wamesisitiza umuhimu wa kuwa na uhusiano thabiti kati ya Washington na Beijing na kusisitiza kuwa mzozo wa aina yoyote kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, unaweza kusababisha matatizo makubwa kimataifa. Kuhusu hilo, Blinken amesema:
" Marekani na China zote zina wajibu wa kusimamia uhusiano huu kwa uwajibikaji. Kufanya hivyo kunalenga maslahi ya Marekani, ya China, na bila shaka ya ulimwengu mzima. "
Hata hivyo viongozi hao wawili wametaja kuridhishwa na hatua zilizofikiwa wakati wa siku mbili za mazungumzo na kubaini kuwa Marekani na China zitarejea katika ajenda pana ya ushirikiano na ushindani ilioidhinishwa mwaka jana na rais Xi Jinping na Joe Biden katika mkutano wa kilele huko Bali, nchini Indonesia.
Soma pia: Hatimaye Blinken akutana na Xi katika ziara yake mjini Beijing
Rais Joe Biden wa Marekani amesema anaamini mahusiano kati ya nchi yake na China yanachukua mwelekeo mzuri na ameashiria kwamba kuna mafanikio kadhaa yaliyopatikana wakati wa ziara ya Blinken huko China ambayo imehitimishwa hapo jana.
Biden amesema Blinken amefanya kazi kubwa iliyowezesha kufikiwa makubaliano ya kusawazisha uhasama baina ya Washington na Beijing kwa dhima ya kuzuia hali hiyo kutogeuka kuwa mzozo.