1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Afghanistan yakamalika Doha bila ufumbuzi

19 Julai 2021

Mazungumzo ya karibuni kati ya serikali ya Afghanistan na Taliban mjini Doha yamemalizika bila mafanikio hata baada ya kiongozi mkuu wa wanamgambo hao wa itikadi kali kusema anaunga mkono kwa dhati suluhisho la kisiasa

https://p.dw.com/p/3wfPF
Katar | Friedensgespräche in Doha
Picha: Media office of Afghanistan High Council for National Reconciliation

Wawakilishi waandamizi wa serikali ya Kabul akiwemo kiongozi wa Baraza Kuu la Maridhiano ya Kitaifa Abdullah Abdullah walikuwa Doha kwa siku mbili za mazungumzo mazito wakati Taliban ikiendelea na operesheni yake kali ya kuyakamata maeneo nchini Afghanistan. Abdullah Abdullah alikuwa na kauli fupi tu baada ya mazungumzo ya jana "Ningetarajia kazi kumalizika usiku huu na ilifanyika, lakini tulikuwa na majadiliano mazuri. sawa? ahsante". Alisema Abdullah Abdullah

Soma pia: Rais Ashraf Ghani kujadili amani ya Afghanistan na viongozi wa kikanda

Katika taarifa ya pamoja, pande hizo mbili zimekubaliana kuhusu haja ya kufikia ufumbuzi wa haki na kukitana tena wiki ijayo. Kiongozi wa Taliban Hibatullah Akhundzada alisema kundi lake limedhamiria kutafuta suluhisho la kumaliza vita licha ya wapiganaji wake kuendelea kukamata maeneo Afghanistan.

Katar | Friedensgespräche in Doha
Pande zote zimekubaliana kukutana tena wiki ijayoPicha: Media office of Afghanistan High Council for National Reconciliation

Lakini mjumbe wa Qatar kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi Mutlaq al-Qahtani anayesimamia mazungumzo ya Doha alisema pande zote zimekubaliana tu kushirikiana kuepusha vifo vya raia, ikiwa.

Wanamgambo hao wa itikadi kali walitumia hatua za mwisho za kuondoka kwa Marekani na wanajeshi wengine wa kigeni kutoka Afghanistan ili kuanzisha msururu wa mashambulizi kasi kote nchini humo. Wanaaminika kudhibiti karibu nusu ya wilaya 400 za Afghanistan, vivuko kadhaa muhimu vya mpakani, na wameizingira miji mikuu ya mikoa kadhaa muhimu.

Msemaji wa vikosi vya usalama vya Afghanistan Ajmal Omar Shinwari amesema wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wamefanya operesheni 244, na kuwauwa wapiganaji maadui 967, wakiwemo makamanda waandamizi. "Watu wa Afghanistan daima wanadai kusitishwa kwa mapigano. Lakini vikosi vya usalama viko tayari kwa amani na vita. Tuko tayari kuwalinda watu wetu. Idadi kubwa ya wilaya zimekombolewa na vikosi vya usalama. Idadi ya jumla ya wilaya zilizokombolewa ni 24".

Soma zaidi: Wanamgambo wa Taliban wakamata miji zaidi Afghanistan

Katika ishara nyingine ya vitisho vinavyoikabili serikali ya Afghanistan, hapo jana ilisema inamuita balozi wake nchini Pakistan na wanadiplomasia wote waandamizi kuhusu "vitisho ya usalama”. Binti ya balozi huyo alitekwa nyara kwa muda katika mji mkuu wa Pakistan Islamabad wiki hii.

Islamabad inapigia debe kuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa kikanda ili kujadili machafuko yanayoendelea baada ya siku kuu ya Eid al-Adha.

AFP