1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Wapalestina, Waisraili yaanza tena

29 Julai 2013

Hatimaye mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina yanaanza tena Washington kwa matarajio ya diplomasia ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, kuweza kupata nafasi ya kufanikiwa mara hii.

https://p.dw.com/p/19FfM
Von rechts: Die israelische Justizministerin Tzipi Livni, US-Außenminister John Kerry und Israels Ministerpräsident Benjamin Netanjahu am 23. Mai 2013 in Jerusalem (Foto: Getty Images) US State of Secretary John Kerry stands with Israeli Defence Minister Boogie Yaalon (L), Minister of International Relations Yuval Steinitz (2L), Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu (C) and Minister of Justice Tzipi Livni (R), at Netanyahu's office on May 23, 2013 in Jerusalem, Israel. (Photo by Uriel Sinai/Getty Images)
Nahost-Friedensgespräche, Netanjahu, Kerry, LivniPicha: Getty Images

Katika makubaliano haya ya aina yake, wakuu wa ujumbe wa mazungumzo kutoka pande zote mbili, wanakutana uso kwa uso leo kuandaa utaratibu wa namna mazungumzo hayo yatakavyokwenda.

Msemaji wa Wizara ya Nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema mkutano huo wa mjini Washington unaweka msingi wa mwanzo wa mazungumzo, akiongeza kwamba pande zinazohusika zitaandaa ratiba ya namna ambavyo hatua za mazungumzo zitapigwa kwenye miezi ijayo.

Waziri wa Sheria wa Isreal ambaye ndiye kiongozi wa nchi hiyo kwenye mazungumzo ya amani na Palestina, Tzipi Livni, akiwa pamoja na msaidizi wake wa masuala ya kisheria, Yitzhak Molcho, watakutana kwanza na kiongozi wa ujumbe wa Palestina, Saeb Erakat, anayeambatana na afisa wa ngazi za juu katika serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mohammed Shtayyeh, katika futari iliyoandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, jijini Washington, jioni ya leo.

Msemaji wa Wizara ya Nje ya Marekani, amesema mikutano ya awali imepangwa kufanyika leo na kesho, Jumanne, huku Kerry akisema viongozi wote wawili wameonesha utayarifu wa kuchukua maamuzi magumu, na amewashukuru kwa kujitolea kwao.

Kuachiwa kwa wafungwa wa Kipalestina

Mazungumzo haya yanakuja siku moja tu baada ya Israel kutangaza kuwaachia huru wafungwa 104 wa Kipalestina, miongoni mwao wakiwa wale waliotiwa hatiani kwa kuwashambuliwa Waisraeli.

Baadhi ya waandamanaji mjini Jerusalem wakipinga kuachiwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina.
Baadhi ya waandamanaji mjini Jerusalem wakipinga kuachiwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina.Picha: Reuters/Ronen Zvulun

Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, alikutana na baraza lake la mawaziri akipigania kuwashawishi baadhi ya washirika wa serikali yake ya mseto kukubaliana na hatua hiyo na ile ya kurejea kwenye mazungumzo na Wapalestina.

"Naamini kurudi kwenye mchakato wa kidiplomasia katika wakati huu ni muhimu kwa taifa la Israel, kwa sababu ya kujaribu kuumaliza kabisa mgogoro huu mrefu na pia kutokana na hali ilivyo kwenye eneo letu, kama inavyooneshwa na changamoto za usalama za Syria na Iran. Makubaliano yoyote yatakayofikiwa kwenye mazungumzo hayo, yatapigiwa kura ya maoni." Aliahidi Netanyahu.

Netanyahu apingwa

Licha ya ahadi hiyo, hatimaye baraza hilo lilipitisha kuachiwa kwa wafungwa kwa kura 12 tu kati ya wajumbe 22, huku saba zikipinga na wawili wakijiepusha kupiga kura zao.

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina.
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina.Picha: Reuters/Issam Rimawi

Naibu Waziri wa Ulinzi anayetokea chama chenye itikadi kali cha Likud, Danny Danon, aliongoza kampeni ya kupinga mpango huo, akisema ni makosa ya kidiplomasia na ya kimaadili.

"Napingana na uamuzi huu. Nadhani Israel hairuhusiwi kuwaachia huru magaidi hao waliowaua Mayahudi. Na nadhani tunaweza kuzungumza na Wapalestina bila ya mambo hayo ya kutisha." Alisema Danon.

Kiongozi wa ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo hayo aliikaribisha kura iliyopigwa na baraza la mawaziri la Israel, akiita hatua muhimu. "Natarajia tutaweza sote kuitumia vyema fursa hii iliyoletwa na juhudi za uongozi wa Marekani", aliliambia shirika la habari la AFP.

Awamu ya mwisho ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Palestina, yaliyoengwaenga na Rais Barack Obama, ilivunjika mwaka 2010 kutokana na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo