1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli iliyosheheni misaada ya chakula yaelekea Gaza

12 Machi 2024

Siku ya pili ya mfungo wa Ramadhani imeingia japo kwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza, hawana furaha kutokana na njaa, magonjwa na kuwa wakimbizi wa ndani, hata hivyo meli iliyosheheni misaada iko njiani kuelekea Gaza.

https://p.dw.com/p/4dQF7
Meli ya shirika la Open Arms la nchini Uhispania ikipakia misaada katika bandari ya Lamaca nchini Cyprus kabla ya kuanza safari kuelekea katika Ukanda wa Gaza
Meli ya shirika la Open Arms la nchini Uhispania ikipakia misaada katika bandari ya Lamaca nchini Cyprus kabla ya kuanza safari kuelekea katika Ukanda wa GazaPicha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Vita katika eneo hilo lililozingirwa vinaendelea kwa zaidi ya miezi mitano sasa huku uingiaji wa chakula na misaada mingine vikipungua kwa kasi. Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeinukuu wizara ya afya ya eneo hilo inayosimamiwa na Hamas ikisema mpaka sasa watu 25 wamekufa kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini, wengi wao wakiwa ni watoto.

Familia ya Wapalestina wakipata futari chini ya majengo yaliyobomolewa katia vita katika eneo la Deir al-Balah.
Familia ya Wapalestina wakipata futari chini ya majengo yaliyobomolewa katia vita katika eneo la Deir al-Balah.Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Wakati huo huo, meli iliyosheheni tani 200 za misaada ya chakula imeanza safari leo hii kutoka Cyprus kuelekea katika Ukanda wa Gaza.

Safari hiyo ni ya majaribio ya kuufikia ukanda wa Gaza kwa njia ya baharini ili kusambaza misaada katika eneo hilo.

Vyakula hivyo vimekusanywa na shirika la hisani la World Food Kitchen ambalo muanzilishi wake ni mpishi mashuhuri José Andrés, aliyeungana na shirika la misaada la Uhispania la Open Arms. Meli hiyo inatarajiwa kufika kwenye ufuo wa Gaza katika muda wa siku mbili hadi tatu zijazo.

Marekani kwa upande wake inapanga kujenga daraja katika eneo la bahari karibu na Gaza ili kufanya shughuli ya kutoa msaada, lakini huenda itachukua wiki kadhaa kabla ya daraja hilo kuanza kutumika.

Vita vilivyochochewa na shambulio la Hamas la Oktoba 7 dhidi ya Israel vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 30,000 huku Umoja wa Mataifa ukiripoti kwamba robo ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na njaa.

Mji wa Khan Younis wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wafuka moshi baada kushambuliwa kwa mabomu Jumatatu 11.03.2024
Mji wa Khan Younis wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wafuka moshi baada kushambuliwa kwa mabomu Jumatatu 11.03.2024Picha: Ismael Mohamad/UPI Photo/IMAGO

Mama mmoja Randa Baker, mkaazi wa Gaza aliyehama nyumbani kwake kwa sababu ya vita amesema katika nyakati za amani, angeliipamba nyumba yake na kuwapikia watoto wake chakula kitamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mama huyo ameongez kusema kuwa haoni kama hii ni Ramadhani,anaona ni kama ni siku ya kawaida tu hafanyi kama inavyotakiwa kwa kuwa hana furaha yoyote. Amesema ameyahama makaazi yake na zaidi ana majonzi na huzuni kwa kuwa uti wa mgongo wa nyumbani kwake yaani mume wake hayuko nao tena.

Idadi ya matukio ya chuki dhidi ya Wahaudi yaongezeka nchini Uswisi

Wakati huo huo, idadi yamatukio ya chuki dhidi ya Wayahudi nchini Uswisi imeongezeka tangu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 nchini Israel na majibu ya baadaye ya serikali ya Israel huko Gaza, haya ni kulingana na ripoti iliyochapishwa Jumanne 12/03/2024.

Utafiti uliofanywa na Shirikisho la Uswisi la Jumuiya za Wayahudi (SIG) na Wakfu wa Kupambana na Ubaguzi na Chuki dhidi ya Wayahudi (GRA) umeonyesha kuwa idadi ya matukio hayo iliongezeka hadi kufikia 155 mnamo 2023. Matukio mengi ni baada ya mashambulio ya Hamas ya Oktoba 7. Matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi nchini Uswisi yalikuwa 57 mwaka uliotangulia.

Vyanzo: RTRE/DPA/AFP