Merkel atetea kurefusha vikwazo vya kupambana na COVID-19
11 Februari 2021Akizungumza bungeni siku ya Alhamis, Kansela Angela Merkel ametoa tahadhari, akisema virusi vilivyojibadilisha maumbile vinaweza kuharibu mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19.
Hotuba ya kansela huyo ilikuwa na lengo la kutetea uamuzi uliochukuliwa na serikali yake kurefusha vikwazo kwa shughuli za maisha vilivyowekwa tangu Novemba mwaka uliopita, hadi Machi saba.
Soma zaidi: Merkel: Maambukizi mapya ya COVID-19 yanapungua Ujerumani
Awali, ilitarajiwa kuwa vikwazo hivyo vingeondolewa tarehe 14 Februari, lakini mkutano wa hapo jana kati ya Kansela Merkel na wakuu wa majimbo 16 yanayounda shirikisho la Ujerumani, uliamua kuwa ni bora kurefusha muda huo, ili kuepuka athari za aina mpya ya virusi iliyojitokeza.
Kila jimbo kuamua kulingana na hali yake ya maambukizi
Kansela Merkel amesema hatua ya kufungua tena shughuli za maisha zitachukuliwa hatua kwa hatua na majimbo kulingana na kiwango cha kushuka kwa maambukizi katika jimbo hilo.
''Hatua inayofuata ya kuondoa vikwazo itachukuliwa na kila jimbo, kwa ikiwa kiwango cha maambukizi kitasalia chini ya visa 35 kwa kila wakaazi 100,000 kwa siku saba mfululizo,'' amesema Kansela Merkel, na kuongeza kuwa kufunguliwa huko kutaanza na maduka ya rejareja, kwa kuheshimu kanuni ya mteja mmoja kwa kila mita 20 za mraba.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya watangaza taratibu kali za kudhibiti mauzo ya chanjo dhidi ya corona
Kulingana na vikwazo vilivyopo sasa nchini Ujerumani, maduka yote yasio ya mahitaji ya lazima yamefungwa, kama ilivyo kwa shule, na wafanyakazi wa maofisini wanahimizwa kufanyia kazi zao nyumbani.
Aina mpya ya virusi yaelezwa kuwa kitisho kikubwa
Wakati hayo yakijiri, mkuu wa kitengo cha kuchunguza vinasaba nchini Uingereza ameonya kuwa kirusi cha corona kilichobadilisha maumbile, ambacho kiligundulika mara ya kwanza katika eneo la Kent nchini humo, ni kitisho kikubwa kwa dunia kwa sababu kinaweza kuhujumu kidhoofisha kinga inayotolewa na chanjo ya COVID-19.
Afisa huyo, Sharon Peacock amesema hadi sasa chanjo ya ugonjwa huo inafanya kazi vyema dhidi ya aina hiyo mpya ya virusi, lakini akaelezea wasiwasi kuwa kadri kinavyozidi kujibadili maumbile, ufanisi wa chanjo hiyo unaweza kutatizika.
Soma zaidi: Ujerumani yarefusha muda wa karantini na yaweka sheria mpya kuhusu uvaaji wa barakoa
Barani Afrika, Kitengo cha Umoja wa Afrika cha kudhibiti magonjwa kinafanya mazungumzo na kampuni ya Johnson & Johnson, ili iuuzie umoja huo dozi zaidi za chanjo ya COVID-19.
Mkuu wa Kitengo hicho, John Nkengasong amesema wanatarajia shehena ya chanjo hiyo itawasilishwa bila kuchelewa barani Afrika, ambako, amesema afisa huyo, majaribio yameonyesha kuwa chanjo nyingine ya AstraZeneca ilikuwa na mafanikio ya kiwango duni, dhidi ya virusi vilivyoenea zaidi nchini Afrika Kusini, vinavyotambuliwa kwa jina la kitalaamu kama 501Y.V2.
Vyanzo: rtre, afpe, https://p.dw.com/p/3pCGk