Merkel atunukiwa Nishani ya Juu ya Taifa
17 Aprili 2023Nishani hiyo yumkini itatoa nafasi kwa wafuatiliaji wa siasa za Ujerumani na umma wa taifa hilo kutathmini kwa kina urathi wa kiongozi huyo wa zamani.
Hafla ya kutolewa nishani hiyo kwa Bibi Merkel inafanyika jioni ya leo mjini Berlin na itakabidhiwa na rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.
Rais wa Ujerumani kwa nafasi yake kama mkuu wa nchi anazo nishani chungunzima ambazo anaweza kuzitoa kwa raia waliojitolea utumishi wao kwa taifa.
Na kwa mujibu wa ofisi ya rais Steinmeier, nishani itakayotolewa leo kwa Merkel ndiyo ya heshima zaidi kuliko nyingine.
Nishani hiyo iliyoanza kutolewa tangu mwaka 1951 hupewa raia wa Ujerumani na hata watu kutoka nje waliowezesha mafanikio ya kupigiwa mfano katika nyanja za siasa, uchumi, jamii na taaluma.
Merkel anakuwa mwanasiasa wa tatu kutunukiwa nishani hiyo
Nishani yenyewe inaitwa kwa kijerumani ´GroßKreuz´- au Msalaba Mkubwa na Bibi Merkel atakuwa mtu wa tatu kupokea aina hiyo ya nishani yenye hadhi ya juu kabisa.
Wengine wawili waliomtangulia nao waliwahi kuwa makansela, ambao Konrad Adenauer, aliyekuwa kiongozi wa kwanza wa Ujerumani baada ya kuanguka utawala wa manazi wa Adolf Hilter. Yeye alitunukiwa nishani mwaka 1954.
Mwengine ni Helmut Kohl, aliyepewa nishani hiyo mwaka 1998 kwa mchango wake wa kuziunganisha tena Ujerumani mbili na kutoa idhini ya kutumika sarafu ya Euro nchini Ujerumani na kuipa kisogo ile iliyowepo ya Deutsche Mark.
Wote hao wawili yaan Adenauer na Kohl walikuwa ni wanasiasa kutoka chama cha Merkel cha Christian Democratic Union, CDU.
Nishani yauweka urathi wa Merkel kwenye mizani
Tangazo la kutolewa nishani hiyo kwa Merkel tayari limezusha mjadala nchini Ujerumani. Wengi wanajaribu kutafuta ulinganifu wa sababu zilizochagiza Merkel kupewa nishani hiyo.
Albrecht von Lucke, mwandishi wa jarida la siasa la Blätter anasema tofauti na watangulizi wake waliolazimika kuchukua maamuzi makubwa ya kisera na kiutawala, Merkel hakufanikiwa kufikiwa viwango hivyo katika uongozi wake wa miaka 16.
Von Lucke anautaja muhula wa Merkel madarakani "kuwa enzi ya miaka 16 iliyopotea" na kwamba kumtunuku nishani hiyo ni uamuzi ulichukuliwa mapema kwa sababu bado haijawa wazi kile utawala wake ulifanikiwa au kushindwa.
Wakosoaji wa Merkel wanamtwika jukumu kwa matatizo kadhaa yanaoikumba sasa Ujerumani.
Tangu kushindwa kutimiza malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hadi mzozo kati ya Urusi na Ukraine ambapo Merkel analaumiwa kwa kuchukua msimamo laini dhidi ya Vladimir Putin na kuifanya Ujerumani kuwa tegemezi kwa Moscow.
Watetezi wa Merkel wanamkingia kifua mwanasiasa huyo wa zamani
Hata hivyo wale wanaotetea rikodi ya Merkel madarakani wanasema sera yake kuelekea Urusi haikuwa na tofauti yoyote na zile za watangulizi wake.
Tangu zamani Ujerumani imekuwa ikapalilia usuhuba na Moscow kwenye Nyanja zote muhimu, tofauti kabisa na mataifa mengine ya Ulaya.
Na yeye mwenyewe Bibi Merkel, alizungumzia hilo mwaka uliopita akisema analaani kwa matamshi makali kabisa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine lakini kamwe hatooomba radhi kwa msimamo wa kisera aliochukua kuelekea Moscow.
Bila shaka yoyote, mjadala kuhusu urathi wa utawala wa Merkel haitamalizika hivi karibuni na uamuzi wa kumtunuku nishani ya juu ya taifa unamrejesha mwanasiasa huyo mbele ya darubini ya wanaomhusudu na wale wanaomkosoa.
Na hilo ni jambo ambalo Bibi Merkel amejaribu kulikwepa sana tangu alipoondoka madarakani.