1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito yaongezeka kuhusu usitishwaji mapigano Gaza

21 Machi 2024

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema wanatarajia kutoa wito wa usitishaji kabisa wa vita, huku mazungumzo ya kuutafutia suluhu mzozo huo wa Gaza yakiendelea nchini Misri.

https://p.dw.com/p/4dz3x
Ukanda wa Gaza- Mashambulizi ya Israel
Uharibifu mkubwa huko Deir al-Balah katika Ukanda wa Gaza: 20.03.2024Picha: Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance

Viongozi hao wa Umoja wa Ulaya ambao wamejumuika katika mkutano wao wa kilele mjini Brussels nchini Ubelgiji,  wanatarajia kutoa wito huo leo. Hayo yameelezwa na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ambaye amesema wamepiga hatua kubwa zaidi kuliko hapo awali.

Borrell amesema wito huo utahusisha kutaka  kusitishwa kabisa kwa mapiganona kuachiliwa kwa mateka, lakini pia kudhihirisha wasiwasi wao mkubwa kwa hali ya watu wa Gaza, ambayo amesisitiza kuwa haikubaliki.

Soma pia: Blinken aendeleza juhudi za suluhu ya vita vya Israel na Hamas

Hayo yakiarifiwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amekutana hii leo mjini Cairo na Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi, ikiwa ni sehemu ya mazungumzo na maafisa wa Kiarabu ili kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza, baada ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusema kamwe hatositisha vita dhidi ya kundi la Hamas.

Saudi Arabia- Waziri  Antony Blinken ziarani Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken (kushoto) akiwa na mwenzake wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan mjini Jeddah, Saudia: 20.03.2024Picha: Saudi Press Agency/REUTERS

Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Saudi Arabia, Qatar, Jordan, na Umoja wa Falme za Kiarabu wamezungumza pia na rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, na miongoni mwa mambo mengine, wamejadili kuhusu kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina na kuhakikisha usalama wa Israel.

Mazungumzo mengine  kuhusu mzozo wa Gaza

Mazungumzo hayo yameanza tena wiki hii nchini Qatar, yakizingatia makubaliano ya takriban wiki sita za usitishwaji mapigano na yangeruhusu kuachiliwa kwa mateka 40 wa Israel na mamia ya Wapalestina waliozuiliwa katika jela za Israel.

Lakini mazungumzo hayo yamekwama kwa kuwa Hamas wanataka usitishwaji kamili wa vita huku Israel ikisema itasaini tu makubaliano ambayo yatazingatia usitishwaji wa muda wa mapigano.

Soma pia: Misri yatoa wito wa misaada zaidi kuingia Gaza kwa njia za ardhini

Katika hatua nyingine, wasiwasi umeongezeka kuhusu kitisho cha kutokea baa la njaa huko Gaza. Wataalam na wanadiplomasia kutoka nchi 36 pamoja na wawakilishi wa mashirika ya misaada ya kimataifa wamekutana nchini Cyprus leo Alhamisi kujadili hatua za uwasilishaji wa misaada zaidi huko Gaza kwa kupitia baharini.

Meli ya misaada kutoka Cyprus ikiwasili Gaza
Meli ya misaada ikitokea katika bandari ya Larnaca nchini Cyprus ikiwasili huko Gaza :15.03.2024Picha: STR/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus Konstantinos Kombos amesema bila hata hivyo kutoa taarifa zaidi, kwamba kikao hicho kilijikita zaidi katika changamoto za masuala ya vifaa vya usafirishaji kutoka bandari ya Cyprus ya Larnaca hadi huko Gaza. Rais wa Cyprus Nikos Christodoulides amesema:

" Kwa vyovyote vile, njia yetu ya baharini, pendekezo letu ni nyongeza kwa njia nyingine za kibinadamu. Na bila shaka, njia zingine zinazowezekana lazima zifunguliwe. Tuko hapa kusaidia mahitaji haya. Hali ya kibinadamu huko Gaza ni mbaya. Tunazungumzia kuhusu mzozo wa kibinadamu na tunahitaji kutumia njia zote zinazowezekana ili kusaidia watu huko."

Soma pia: Meli ya misaada kutoka Cyprus taratibu yakaribia Gaza

Serikali ya Cyprus imesema meli iliyosheheni takriban tani 500 za vifaa vya msaada imeegesha katika bandari ya Larnaca tayari kwa kuondoka mnamo siku chache zijazo. Hii itakuwa shehena ya pili ya msaada utakaowasili Gaza kwa kutumia njia ya bahari. Siku ya Jumamosi, meli ya shirika la misaada iliwasilisha takriban tani 200 za msaada. Larnaca inapatikana takriban kilomita 400 kutoka Ukanda wa Gaza.

(Vyanzo: Mashirika)