Mjumbe wa Ujerumani kuhusu Ebola azuru Liberia
9 Desemba 2014Katika mahojiano na mwandishi wa DW mjini Monrovia Julius Kanubah, bwana Lindner amesema ipo dalili njema kwamba kitisho cha ugonjwa huo kinapungua, na kuonya lakini kwamba huu sio wakati wa kulegeza kamba.
Mahojiano hayo yalifanyika baada ya mjumbe huyo wa Ujerumani kuhusu Ebola, Walter Lindner kuizuru hospitali ya John F Kennedy ambayo ndio kubwa zaidi nchini Liberia. Karibu na hospitali hiyo Ujerumani imekiweka kituo cha kisasa ambacho kinatumiwa kuwapima watu wanaoingia hospitalini humo, na kuwatenga wale wenye dalili za Ebola ili wakashughulikiwe katika kituo kilichojengwa mahsusi kwa ajili hiyo.
Kituo hicho kilijengwa baada ya kubainika kwamba wagonjwa wengi walikuwa wakisusia kuja katika hospitali hiyo kwa hofu kwamba wanaweza kuondoka na maambukizi ya maradhi ya Ebola. Katika mahojiano na mwandishi wa DW Julius Kanubah, Walter Lindner alisema kituo hicho ni miongoni mwa huduma nyingi ambazo Ujerumani imechangia katika mapambano dhidi ya Ebola.
''Kituo hiki kinahitaji vifaa vya kutosha na vya kisasa, na hilo ndilo jukumu la wanajeshi wa Ujerumani, na wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu la Ujerumani. Pamoja na hayo lakini, wanafanya vile vile kazi nyingine za kiufundi, kama kuweka mitambo ya kuzalisha umeme ili kuiwezesha hospitali hii kufanya kazi kwa ufanisi zaidi hata baada ya kitisho cha Ebola kumalizika.'' Amesema Lindner.
Fungu la Euro milioni 150
Lindner amesema Ujerumani imetumia kiasi cha Euro zipatazo milioni 150 katika shughuli za kupambana na Ebola. Amesema fedha hizo zimetumiwa kugharimia safari za ndege za jeshi la Ujerumani kati ya miji ya nchi tatu za Afrika Magharibi zilizoathirika zaidi, yaani Liberia, Sierra Leone na Guinea, zikisafirisha madawa na chakula cha msaada, ambacho kinatolewa na mashirika ya msaada ya Ujerumani.
Safari za kuwapeleka baadhi ya wagonjwa barani Ulaya kupata matibabu zaidi pia hugharimiwa na fuko hilo lililotolewa na Ujerumani.
Msaada uliotolewa na Ujerumani unajumuisha pia mafundi stadi 20 wanaokarabati vifaa vya matibabu, na pikipiki 400 ambazo zina majokofu yanayotunza damu za wagonjwa wakati zikipelekwa katika maabara kuchukuliwa vipimo.
Matumaini ya kupatikana mafanikio
Hii ni safari ya tatu ya kikazi aliyoifanya magharibi mwa Afrika Walter Lindner tangu alipoteuliwa kuchukua majukumu hayo, na amesema hali imeboreka kwa wakati huu, hususan nchini Liberia, ikilinganishwa na wakati alipokuwa huko wiki sita zilizopita.
Amesema wakati huo kilio kilikuwa ukosefu wa vitanda kwa sababu wagonjwa walikuwa wengi, lakini kwa sasa vitanda vingi ni vitupu. ''Hali hii inaleta matumaini kwamba mapambano dhidi ya Ebola yanafanikiwa'', amesema mjumbe huyo wa Ujerumani, na kuonya lakini kwamba huu sio wakati wa kupunguza kazi ya kupambana nao ikitiliwa maanani kwamba msimu wa Krismasi unakaribia, ukiambatana na hofu kuwa pengine sherehe zake zinaweza kuongeza kiwango cha mawasiliano baina ya watu na hivyo kuzidisha maambukizi ya Ebola.
Alipoulizwa maoni yake kuhusu kuchelewa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuitikia wito wa kusaidia mataifa ya Afrika Magharibi kupambana na Ebola, Walter Lindner amesema lililo muhimu kwa wakti huu ni kuutokomeza, na kwamba muda mwafaka wa kufanya tathmini kama hizo utakuwa wakati watu wa eneo hilo watakapokuwa hawakabiliwi tena na kitisho cha Ebola.
Mwandishi: Daniel Gakuba/Interview
Mhariri:Josephat Charo