Mkutano wa APEC wagubikwa na mizozo ya mipaka
8 Septemba 2012Mada kubwa kwenye meza ya viongozi wa eneo hilo ni kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi 21 wanachama. Hata hivyo, mkutano wa mwaka huu unafanyika kukiwa na mzozo wa mpaka unaozihusisha nchi kubwa katika jumuiya hiyo.
Kumekuwepo na mgogoro unaozihusisha China, Japan na Korea Kusini kuhusu mipaka, ambayo imachochea hisia kali za kizalendo katika mataifa hayo. Uhusiano baina ya China na Marekani pia umeathiriwa na tofauti juu ya madai ya China katika bahari ya China Kusini.
China yanyoosha mkono wa amani
Akizungumza katika kongamano la kibiashara mjini Vladivostok kabla ya mkutano wa kilele kuanza, rais wa China Hu Jintao amezitolea wito nchi zote zinazohusika kuhakikisha kuwa mivutano hiyo haisababishi uhasama.
''Kuhakikisha utengamano na ukuaji wa uchumi katika eneo la Asia Pasifiki ni jukumu la kila nchi, na ni kwa maslahi ya kila nchi ya eneo hilo'' Alisema Hu.
Philippines na Vietnam zinaishutumu China kutumia vitisho katika kampeni yake kujinyakulia eneo zima la Bahari ya China Kusini ambayo inadai ni lake. Wakati huo huo Marekani imeikasirisha China kwa kutoa wito wa kuwepo kanuni zinazoheshimiwa na nchi zote katika eneo linalozozaniwa, na uhuru wa safari za majini katika sehemu za Bahari ya China Kusini ambazo Marekani inazichukulia kwa za kimkakati kwa maslahi yake.
Marekani yasema haimuombi radhi mtu
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton ambaye anamwakilisha Rais Barack Obama katika mkutano wa Vladivostok, amesema hataomba radhi kwa kuendeleza maslahi ya nchi yake katika eneo la Asia-Pasifiki. Katika hatua nyingine ya kuzidisha mvutano, waziri mkuu wa Japan Yoshihiko Noda amesema hatafanya mazunguzo yoyote na marais wa China na Korea Kusini, nchi ambazo zina mizozano ya muda mrefu na Japan kuhusu umilikaji wa visiwa.
Tofauti kati ya China na Japan zilifikia kiwango kipya mnamo wiki zilizopita, baada ya vyombo vya habari vya Japan kusema serikali ya nchi hiyo ilikuwa inaazimia kununua visiwa vinavyozozaniwa kati yake na China, kutoka kwa matajiri wa Japan ambao wanavimiliki visiwa hivyo.
China ilijibu kwa kutishia kuchukua hatua ''zozote' zinazohitajika kulinda haki yake kumiliki visiwa ambavyo inavitambua kama Diaoyu. Visiwa hivyo nchini Japan vinajulikana kama Senkuku.
Mkutano utasonga mbele
Licha ya mizozo hiyo lakini, viongozi kwenye mkutano huo wa kilele wamesisitiza kuwa kitakachopewa kipaumbele ni kufungua milango ya kibiashara miongoni mwa nchi za eneo la Asia-Pasifiki, ambazo kwa pamoja zinashikilia asilimia 44 ya biashara zote duniani.
Urusi imetumia dola bilioni 20 kuukarabati mji wenye bandari wa Vladivostok unakofanyika mkutano huo, kwa malengo ya kuufanya kuwa kitovu cha uwekezaji na malengo yake katika eneo la Pasifiki.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo