1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras kuwasilisha mapendekezo

7 Julai 2015

Mkutano wa dharurua wa viongozi wa kanda ya sarafu ya Euro kuujadili mzozo wa kiuchumi wa Ugiriki unafanyika leo, baada ya nchi hiyo kupiga kura ya maoni kukataa mpango wa kubana matumizi, uliopendekezwa na wakopeshaji.

https://p.dw.com/p/1Fttc
Kansela Merkel na Rais Hollande
Kansela Merkel na Rais HollandePicha: Getty Images/B. Guay

Wakati uchumi wa Ugiriki ukisuasua, na mabenki yakikaribia kufungwa siku ya Alhamisi kutokana na wasiwasi wa ukosefu wa fedha kwenye mashine za kutolea pesa, Ujerumani na Ufaransa zimeitaka serikali ya Tsipras kuwasilisha mapendekezo madhubuti katika jitihada za kujaribu kuyafufua tena mazungumzo ya kuusaidia uchumi wa nchi hiyo.

Baada ya kufanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema mlango wa mazungumzo uko wazi.

''Mlango bado uko wazi kwa mazungumzo, lakini ni muhimu sasa kwa Waziri Mkuu Tsipras kutoa mapendekezo madhubuti na ya kuaminika ili utayari wa kubakia kwenye kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro utafsiriwe kama mpango wa kudumu,'' alisema Hollande.

Mazungumzo ya viongozi hao yalifanyika hapo jana, siku moja baada ya Wagiriki kuyakataa masharti magumu yaliyopendekezwa na wakopeshaji wa kimataifa katika kura ya maoni ya kihistoria. Matokeo ya kura hiyo ni ushindi mkubwa wa kisiasa kwa Tsipras, lakini umeitumbukiza Ulaya kwenye mzozo.

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis TsiprasPicha: Getty Images/Greek Prime Minister's Office

Kwa upande wake, Kansela Merkel amesema masharti mapya kwa ajili ya kuuokoa uchumi wa Ugiriki bado hayajafikiwa na ndiyo maana wanasubiri mapendekezo sahihi kutoka kwa Tsipras, mpango ambao utairuhusu Ugiriki kurejea kwenye mafanikio. Amesema kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro tayari yameonyesha mshikamano mkubwa kwa Ugiriki.

Muda unayoyoma

''Muda unakimbia, hivyo mapendekezo kama hayo yanapaswa kuwasilishwa haraka wiki hii, ili tuweze kuutatua mzozo uliopo,'' alisisitiza Merkel.

Naye Kamishna wa Uchumi wa Kidigitali wa Umoja wa Ulaya, Gunther Oettinger ameviambia vyombo vya habari vya Ujerumani kwamba bila ya kuwa na mapendekezo yoyote, mazungumzo yoyote yale mapya yatakuwa hayana maana.

Aidha, Waziri mpya wa Fedha wa Ugiriki, Euclid Tsakalotos amesema nchi yake ingependa kuendelea na mazungumzo na wakopeshaji wake. Tsakalotos aliteuliwa jana kushika nafasi ya Yanis Varoufakis aliyejiuzulu wadhifa huo mapema jana asubuhi.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: P. Hertzog/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker leo amesema hangependa kuiona Ugiriki inajiondoa kwenye kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro. Akizungumza katika Bunge la Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Ugiriki ilipopiga kura yake ya maoni kuyakataa mapendekezo ya wakopeshaji wa kimataifa, Juncker amesema hakuna mtu yeyote anayepaswa kufikiria kuiondoa Ugiriki kwenye kanda hiyo.

Ikulu ya Marekani imezitaka pande zote kutafuta muafaka utakaosaidia kuifanya Ugiriki kuurejea katika njia itakayofanikisha nchi hiyo kukua kiuchumi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman