Mkutano wa G7 wajadili vita vya Ukraine na Gaza
25 Mei 2024Kundi la Mataifa tajiri ulimwenguni la G7 limesema linajadiliana juu ya namna watakavyotumia mapato ya baadaye ya mali za Urusi walizozizuia ili kuisaidia Ukraine ambayo inakabiliana na uvamizi wa Urusi.
Wakuu wa taasisi za kifedha wa kundi hilo wamesema hayo siku ya Jumamosi (25.05.2024), hii ikiwa ni kulingana na rasimu ya taarifa ambayo shirika la habari la Reuters limepata nakala yake.
Kundi la G7 limezuia mali za Urusi zenye thamani ya dola bilioni 300, muda mfupi tu baada ya kuivamia Ukraine, Februari 2022. Duru kutoka kwenye kundi hilo zimesema rasimu hiyo haitafanyiwa marekebisho makubwa kabla ya toleo la mwisho kutangazwa rasmi baadae leo.
Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amesema kuipatia mkopo Ukraine kwa kutumia mapato ya mali za Urusi zilizozuiwa ni "chaguo muhimu" ambalo viongozi wa G7 wanatakiwa kulizingatia mwezi Juni lakini akaongeza kuwa hana nia ya " kuondoa mapendekezo mengine yanayowezekana katika siku zijazo". Pendekezo hilo litahitajika kuidhinishwa na wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya.
Msimamo wa Urusi na wasiwasi kuhusu China
Waziri wa Fedha wa Urusi Anton Siluanov amesema siku ya Jumamosi kwamba Urusi itajibu ikiwa mataifa ya magharibi yatatumia mali zake kinyume cha sheria.
Shirika la habari la Urusi TASS lilinukuu kauli ya Waziri Siluanov wakati alipokuwa akitoa maoni yake juu ya mpango unaojadiliwa na Mawaziri wa Fedha wa G7 wanaolenga kutumia mapato yatokanayo na mali za Urusi zilizozuiwa ili kuisaidia Ukraine.
Mbali na Urusi, viongozi hao wa G7 wameelezea pia "wasiwasi" wao juu ya sera za biashara za China, wakisema watazingatia hatua "zitakazohakikisha uwezo sawa" kwa uchumi wa mataifa yote.
Soma pia: G7 kuangazia namna ya kutumia mali za Urusi ilizozizuia ili kuisaidia Ukraine
Katika rasimu ya taarifa yao baada ya mazungumzo huko Stresa kaskazini mwa Italia, mawaziri hao wa G7 wamesema: "Tutaendelea kufuatilia athari hasi zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokuwa na sheria za usawa na tutazingatia kuchukua hatua ili kuhakikisha hilo linafikiwa kwa mujibu wa kanuni za Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO).”
Viongozi wa G7 wavijadili pia vita vya Gaza
Mawaziri wa fedha wa G7 wanatarajia kuitoa wito Israel kutovuruga "mifumo muhimu ya kifedha" katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kufuatia dalili kwamba inaweza kukata mawasiliano na benki za Mamlaka ya Palestina.
Rasimu ya taarifa ya viongozi hao ambayo shirika la habari la AFP limepata nakala yake imesema: " Tunatoa wito kwa Israel kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha kuwa huduma za kibenki kati Israel na Palestina zinaendelea kuwepo, ili miamala muhimu ya kifedha, biashara na huduma muhimu ziendelee."
Mawaziri wa G7 waliokusanyika huko Stresa wameitolea pia wito Israel "kuipatia Mamlaka ya Palestina mapato yaliyozuiwa, kwa kuzingatia mahitaji yake ya haraka ya kifedha", na wameitaka Israel "kuondoa au kulegeza hatua zingine ambazo zimeathiri vibaya biashara ili kuepusha kuzidisha hali mbaya ya uchumi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu".
Siku ya Jumatano wiki hii, Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich alisema nchi yake haina mpango wa kurefusha mpango muhimu kati ya taasisi za kifedha za Israel na Mamlaka ya Palestina, ambao unatarajiwa kufikia tamati katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo.
Marekani ilielezea wasiwasi wake na kuonya juu ya uwezekano wa hatari ya "mgogoro wa kibinadamu" ikiwa hilo litatokea. Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amesema mifumo hiyo ya kibenki ni muhimu kwa shughuli mbalimbali zenye thamani ya karibu dola bilioni 8 kwa mwaka ikiwa ni pamoja na bidhaa kutoka Israel, umeme, maji, mafuta na chakula." Pia mifumo hiyo huwezesha "karibu dola bilioni 2 kwa mwaka katika mauzo ya nje ambayo ni muhimu mno kwa maisha ya mamilioni ya Wapalestina.
(Vyanzo: AFP, AP, RTR, DPA)