Mkutano wa NATO: G7 yatoa ahadi kwa Ukraine
13 Julai 2023Mkutano huo wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami NATO umemalizika huku suala la kufahamu ni lini Ukraine itajiunga rasmi na muungano huo wa kijeshi likiwa halikupatiwa ufumbuzi na viongozi hao wakishindwa kuipatia nchi hiyo tarehe ya uhakika ya kukaribishwa ndani ya Jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Viongozi wa kundi la mataifa tajiri duniani, G7 na wale wa Umoja wa Ulaya waliokutana pembezoni mwa mkutano wa NATO huko Vilnius, Lithuania wametangaza mpango wa kimataifa wa kuendelea kuisaidia Ukraine kijeshi na kuipatia uwezo mkubwa wa kuweza kujilinda na kujihami. Mpango huo unatoa dhamana ya usalama ya muda mrefu kwa Ukraine ili kudhibiti uchokozi wa Urusi wa siku zijazo.
Katika mpango wa pamoja, ambao unatoa fursa kwa mataifa mengine kushiriki, viongozi wa G7 kutoka Marekani, Ujerumani, Japan, Ufaransa, Canada, Italia na Uingereza, pamoja na Umoja wa Ulaya, wamesema kuwa mpango huo wa kuisaidia Ukraine utajumuisha vifaa na mafunzo ya kijeshi, kubadilishana taarifa za kijasusi, na teknolojia ya ulinzi wa mtandaoni. Rais wa Marekani Joe Biden amesema G7 itaisaidia Ukraine kuimarisha jeshi lake wakati ikisubiri kujiunga na NATO.
Soma pia: Mataifa ya G7 yaahidi kupeleka silaha kwa muda mrefu kuisaidia Ukraine katika vita vyake na Urusi
Nchi kadhaa tayari zimetia saini kuunga mkono mpango huo wa G7, zikiwemo Uhispania, Uholanzi, Ureno, Iceland, Norway, Denmark, Poland na Jamhuri ya Czech. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema mshikamano huu wa kimataifa unaonyesha kuwa Ukraine inaungwa mkono kwa muda mrefu huku Urusi, iliyokabiliwa hivi karibuni na uasi wa muda mfupi wa kundi la mamluki la Wagner, ikiwa katika hali tete kijeshi na kisiasa na kusema hii inadhihirisha wazi dalili za mwanzo za mgawanyiko.
Kwa upande wake Ukraine itatakiwa kuboresha sera zake ikiwa ni pamoja na mageuzi ya kimahakama na kiuchumi na vilevile kuzidisha uwazi katika utawala wake. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema makubaliano hayo ni ushindi mkubwa wa usalama kwa Ukraine, lakini pia akataja kusikitishwa na kukosekana kwa hatua ya wazi kuhusu nchi yake kujiunga rasmi na NATO.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imesema hapo jana kuwa mkutano huo wa NATO unaonesha kuwa muungano huo wa kijeshi ulikuwa ukirejea kwenye mikakati ya Vita Baridi, na kwamba Urusi itakuwa tayari kujibu vitisho na kwa kutumia kila njia. Hivi majuzi Moscow ilikemea kitendo cha NATO kuzidisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kusema kuwa hatua hizo zinavileta karibu mno Vita vya Tatu vya Dunia.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeendelea kusema katika taarifa iliyotolewa usiku wa jana kuwa matokeo ya mkutano wa Vilnius yatachambuliwa kwa makini kwa kuzingatia maslahi, changamoto na vitisho vya usalama dhidi ya Urusi na kwamba watajibu kwa wakati muafaka na kwa njia inayofaa, kwa kutumia mifumo na mbinu zote walizo nazo.
Soma pia: Urusi yaishutumu N ATO kwa uadui
Rais wa Marekani Joe Biden ambaye tayari amewasili nchini Finland, ambayo imekuwa nchi ya hivi karibuni kujiunga na NATO, amemshutu Rais wa Urusi Vladmir Putin kuwa mwenye tamaa kubwa ya ardhi na madaraka huku akipongeza hatua zote zilizochukuliwa na NATO.