Mkutano wa NATO waanza Wales
4 Septemba 2014Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko anatarajiwa kuwahutubia viongozi wa dunia kwenye mkutano huo wa siku mbili unaofanyika kwenye mji wa Newport, Wales, utalenga zaidi kuujadili mzozo wa Ukraine na kuimarisha mikakati ya kuilinda Ulaya ya Mashariki, huku viongozi wa dunia wakitarajiwa kuonyesha umoja na mshikamano dhidi ya uchokozi unaofanywa na Urusi.
Jumuiya hiyo inatafuta njia za kuwahakikishia ulinzi wa kutosha wanachama wake wa Ulaya Mashariki bila kuikasirisha Urusi. Jana, Rais Barack Obama wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake itaongeza uwepo wa majeshi yake kwenye mataifa ya Baltic. Obama na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, wameapa kuisaidia Ukraine.
Poroshenko kuhutubia Baraza la NATO na Ukraine
Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko atakihutubia kikao cha Baraza la NATO na Ukraine, lililoanzishwa baada ya nchi hiyo kuwa mshirika wake mnamo mwaka 1997. Poroshenko atawaarifu viongozi wa dunia kuhusu mazungumzo yaliyofanyika jana Jumatano kati yake na Rais wa Urusi, Vladmir Putin, ambayo yameonyesha kupiga hatua kubwa kuelekea katika kusitisha mapigano na kupatikana kwa amani ya kudumu mashariki mwa Ukraine.
Poroshenko amesema ana matumaini makubwa ya kufikiwa kwa makubaliano katika mkutano utakaofanyika kesho huko Minsk. Jana, Rais Putin alisema makubaliano ya kusitisha mapigano yanaweza yakafikiwa kwenye mkutano huo, baada ya kutoa mpango wenye masharti saba kwa ajili ya kufikiwa kwa mkataba. Hata hivyo, mpango huo ulikataliwa na Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema hapatokuwa na kikosi cha kudumu cha majeshi ya NATO Ulaya ya Mashariki, lakini jumuiya hiyo itayalinda mataifa ya Baltic ya Latvia, Lithuania na Estonia. Merkel amesema Urusi inapaswa kuheshimu uhuru wa mataifa ya Baltic.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen amesema leo kuwa Urusi inaivamia Ukraine. Amesema anadhani Urusi hawana nia ya dhati ya kusitisha mapigano na wanataka kuendelea kudhoofisha usalama wa mashariki mwa Ukraine.
NATO kuisihi Urusi kuondoa majeshi yake mpakani
Amesema NATO inaendelea kuisihi Urusi kuondoa majeshi yake kwenye mpaka wa Ukraine, kuacha kupeleka silaha na wapiganaji Ukraine, kuacha kuwaunga mkono waasi wenye silaha na kushiriki kwenye mazungumzo yenye tija ya kisiasa.
Hata hivyo, Rasmussen amesema NATO imepokea kwa furaha juhudi za kutafuta amani ya mashariki mwa Ukraine inayofanywa na Putin, lakini wanazingatia zaidi kile kinachoendelea kwenye eneo hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ameionya NATO kuhusu kuipatia Ukraine uwanachama wa jumuiya hiyo. Lavrov pia ameitaka Ukraine na waasi wanaoiunga mkono Urusi kuunga mkono juhudu za amani zilizopendekezwa na Putin.
Licha ya juhudi za kusaka amani kuendelea, maroketi yamerushwa kuelekea kusini mwa ngome ya waasi ya Donetsk, usiku wa kuamkia leo. Maeneo ya kaskazini mwa mji huo, pia yaliandamwa na mashambulizi jana. Hata hivyo, bado hakuna taarifa za kuwepo vifo kwenye wilaya ya Petrovka, ingawa mpiganaji wa waasi amedai kuwa watu kadhaa wameuawa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga