Mkuu wa jeshi la Pakistan azungumzia hali ya Musharraf
1 Mei 2013Hapo jana mahakama ya Pakistan ilimpiga marufuku Pervez Musharraf kushiriki katika uchaguzi wowote nchini humo kwa maisha yake yote. Hii inamaanisha kwamba Musharraf hatoweza tena kujiingiza katika siasa za nchi hiyo kwa kuwa hawezi kushiriki katika uchaguzi wa aina yoyote.
Musharraf mkuu wa zamani wa jeshi la Pakistan alirejea nchini mwake mwezi Machi baada ya kukaa uhamishoni kwa takriban miaka minne ili baadaye aweze kushiriki katika uchaguzi mkuu wa May 11. Hata hivyo maafisa wa uchaguzi wameizima ndoto yake hiyo, wakisema Musharraf anakabiliwa na kesi nyingi mahakamani.
Kwa sasa jenerali mkuu wa jeshi Ashfaq Kayani amesema kwa maoni yake, kulipiza kisasi sio jambo muhimu ila kuhamasishana na kushiriki kwa wingi ndio njia moja ya kumaliza mchezo wa siku nyingi na kuweka wazi kati ya maswala ya demokrasia na yale ya udikteta.
Pakistan imetawaliwa kijeshi katika nusu ya miaka 66 ya historia yake, kutokana na mapinduzi ya mara kwa mara. Jeshi limekuwa likiunda sera za usalama na za kigeni hata wakati kukiwa na serikali iliochaguliwa na wananchi.
Mahakama yatoa amri ya kukamatwa kwa Musharraf
Mwezi uliopita mahakama iliamuru kukamatwa kwa Musharraf kutokana na makosa aliyoyafanya mwaka wa 2007 alipokuwa madarakani ya kuwafuta kazi majaji watatu na kutaka kuwaweka katika kifungo cha nyumbani.
Hii ni kufuatia jaji Iftikhar Chaudhry, kupinga mipango ya Musharaff kutaka kuongeza muda wa kutawala alipokuwa rais wa nchi hiyo.
Musharraf pia anakabiliwa na mashitaka ya kupanga njama ya mauaji ya kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto mwaka wa 2007, na kuhusiana na kifo cha kiongozi wa waasi kabila la Baluchi wakati wa operesheni ya kijeshi mwaka wa 2006.
Uchaguzi mkuu nchini Pakistan unatarajiwa kufanyika tarehe 11 mwezi huu huku jenerali mkuu wa jeshi Ashfaq Kayani akisema kwamba, jeshi litahakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani licha ya mashambulizi ya hivi hivi karibuni yaliowalenga wanasiasa na kusababisha watu 61 kuuwawa tangu Aprili 11.
Uchaguzi ujao utaashiria kukamilika kipindi cha kwanza cha mpito cha kubadilishana madaraka kwa njia ya kidemokrasia baada ya serikali iliochaguliwa na raia na kumaaliza muda wake hivi karibuni kufanikiwa kukaa madarakani kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman