Mkuu wa NATO ataka mapigano yasitishwe Nagorno-Karabakh
5 Oktoba 2020Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev amesema leo kuwa ni sharti Uturuki ihusishwe kwenye mchakato wa kutafuta amani ya eneo lenye machafuko la Nagorno-Karabakh. Naye Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameitaka Uturuki kutumia ushawishi wake ili kumaliza mvutano katika eneo hilo.
Machafuko kati ya Azerbaijan na Armenia yameingia siku ya tisa leo huku mapigano makali yakishuhudiwa kuhusu eneo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh.
Msemaji wa jeshi la Armenia Shushan Stepanyan amesema kwenye taarifa kwamba vita vikali vinaendelea.
Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi mjini Baku imesema vikosi vya Armenia vimeushambulia mji wa pili kwa ukubwa wa Azerbaijan Ganja, huku makombora yakifyatuliwa kutoka eneo la Berd, kaskazini magharibi mwa Armenia.
NATO yaitolea Uturuki wito kuingilia kati machafuko ya Nagorno-Karabakh
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesema jumuiya hiyo ya kijeshi ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ilivyo ndani na nje ya eneo la Nagorno-Karabakh, hususan kuhusu ongezeko la idadi ya wanaouawa, wakiwemo raia, pamoja na kitisho dhidi ya miundo mbinu muhimu.
Jens Stoltenberg ambaye amezungumzia machafuko hayo akiwa mjini Ankara nchini Uturuki akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Mevlut Cavusoglu, ameitolea wito Uturuki kutumia ushawishi wake kuyatuliza machafuko hayo na pia amezitaka pande zote kusitisha mapigano mara moja.
Soma pia: Usitishwaji mapigano Nagorno-Karabakh
"Ni muhimu zaidi kwetu kuwasilisha ujumbe wa wazi kabisa kwa pande zote zinazohusika kwamba zinapaswa kusitisha mapigano mara moja, kwamba tunapaswa kuunga mkono juhudi zote za kupata suluhisho la amani kwa mazungumzo kwa sababu hakuna suluhisho la kijeshi ndani na hata nje ya Nagorno-Karabakh." Amesema Stoltenberg.
Zaidi ya watu 200 wameuawa katika siku 9
Mkuu huyo wa Jumuiya ya NATO anatarajiwa kukutana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye amevitaka vikosi vya Armenia kuondoka katika eneo linalokaliwa kimabavu la Azerbaijan ili amani idumu.
Viongozi wa kikabila wa Armenia katika eneo hilo la machafuko wamesema kuwa wanajeshi wengine 21 wameuawa leo.
Zaidi ya watu 200 wameuawa tangu machafuko hayo ya hivi karibuni, na ndiyo mabaya zaidi miongoni mwa machafuko kati ya majirani hao katika miaka minne iliyopita.
Uhasama huo unatokana na nini?
Eneo la Nagomo-Karabakh linazingatiwa na Umoja wa Mataifa kama sehemu ya Waislamu wa Azerbaijan, lakini kwa miongo mingi limekuwa likikaliwa na wanajeshi Wakristo wa Armenia.
Machafuko ya hivi karibuni katika eneo hilo yamezusha hofu kuwa yanaweza kugeuka kuwa vita vibaya huku pande zote zikitafuta usaidizi kutoka kwa mataifa ya nje, Uturuki na Urusi.
(DPAE, RTRE, AFPE, APE)