Mkuu wa WFP aelezea wasiwasi kuhusu usalama wa chakula
5 Machi 2021Akiwa ziarani mjini Kinshasa Beasly amesema WFP itaendesha miradi ya kusambaza misaada. David Beasley alikuwa na mashauriano na rais Felix Tshisekedi ambae pia ni mwenye kiti wa sasa wa Umoja wa Afrika. Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya rais Tshisekedi, mkuu huyo wa shirika la Mpango wa Chakula Duniani alielezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa chakula na athari hasi za janga la Covid-19 nchini Congo na kwenye baadhi ya nchi barani Afrika.
Mradi wa kusambaza chakula
Beasley amesema bara la Afrika linakabiliwa na uhaba wa chakula unaotokana kwa nafasi kubwa na janga la virusi vya Corona. Ameongeza kuwa kabla ya janga la Covid-19 kulikuwepo na watu milioni 140 waliokumbwa na uhaba wa chakula, lakini hivi sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia watu milioni 270 .
David Beasley ameomba kuwepo na juhudi za pamoja za viongozi wa Kiafrika katika kukabilana na baa la njaa. Mkuu huyo wa shirika la Mpango wa Chakula Duniani, ametangaza kuwa WFP litaendesha mradi wa kusambaza chakula nchini Congo na ambao utagarimu dola bilioni 1.6.
Ziara hiyo imekuja siku 10 baada ya shambulizi dhidi ya msafara wa shirika la WFP huko Goma. Shambulizi hilo la watu wenye silaha lilisababisha kifo cha balozi wa Italia nchini Congo, mlizi wake pamoja na dereva wa shirika la WFP.
''Kwa pamoja tunatakiwa kurejesha amani''
Wakati huohuo kiongozi mpya wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Monusco, Bintou Keita amesema kuna umuhimu wa ushirikiano wa dhati baina ya Congo na Monusco kurejesha usalama hasa kwenye majimbo ya Kivu. Bintou aliyasema hayo kufuatia mashauriano yake ya kwanza na rais Felix Tshisekedi.
'' Monusco bado iko hapa ili kuunga mkono juhudi za viongozi wa Congo. Kwa pamoja tunatakiwa kurejesha amani na kuhakikisha ustawi wa eneo la mashariki. Tunaomba juhudi za pamoja na ushirikiano.'', alisema Bintou.
Bintou Keita, raia wa Guinea, aliwasili mjini Kinshasa Jumatano ilikuchukua rasmi uongozi wa ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya Mwafrika mwengine Leila Zerrougui kuondoka.