1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MONUSCO yaanza kuondoka mashariki mwa Kongo

28 Februari 2024

Umoja wa Mataifa umeanza hatua ya kuviondoa vikosi vyake vya kulinda amani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutekeleza matakwa ya serikali ya nchi hiyo ambayo inakiangalia kikosi hicho kama kilichoshindwa.

https://p.dw.com/p/4czat
Maandamano dhidi ya MONUSCO
Maandamano ya kupinga kuwapo kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Hatua ya kwanza ya Umoja huo imekuwa kuikabidhi polisi ya taifa la Kongo kambi iliyokuwa ikitumiwa na MONUSCO iliyoko Kamanyola karibu na mpaka wa taifa hilo na Burundi.

MONUSCO inatarajiwa kukabidhi kambi zake zote 14 zilizoko mkoa wa Kivu Kusini kwa vikosi vya Kongo kabla ya mwezi Mei.

Soma zaidi: Wafanyakazi wa MONUSCO washambuliwa mjini Kinshasa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilishinikiza kuondolewa kwa vikosi hivyo, licha ya wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kuhusu machafuko ambayo yamekithiri mashariki mwa taifa hilo.

Serikali mjini Kinshasa inashikilia kuwa vikosi vya MONUSCO vimeshindwa kuwalinda raia dhidi ya makundi yenye silaha na wanamgambo ambao wamekuwa wakishambulia mashariki mwa Kongo kwa miongo mingi.