1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msisimko wa Bundesliga

8 Agosti 2011

Bayern Munich baada ya kishindo walichopania kuanza msimu mpya wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga, ilifungwa 1-0 na timu ya Borussia Monchengladbach kutokana na makosa kati ya wachezaji wawili wapya timu hiyo inayojivunia

https://p.dw.com/p/12D25
Kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer amebaki na laitiPicha: dapd

Waswahili wanakwambia vishindo vya mashua havishutui bahari!

Bao la pekee lililoipa Monchengladbach ushindi lilikuwa ni la Igor de Camargo aliyepatiliza mchanganyiko uliotokea kati ya kipa Manuel Neuer na mlinzi Jerome Boeteng.

Jerome Boateng wechselt zum FC Bayern München
Nyota mpya ya Bayern Munich, Jerome BoatengPicha: picture-alliance/GES-Sportfoto

Kocha wa Bayern mwishowe alieleza kuwa timu hiyo pinzani ilikuwa imejipanga vizuri, na iliunda mtandao ambao kwa kawaida Bayern hunaswa.

Kwengineko timu ya Bayer Leverkusen walioinyakuwa nafasi ya pili msimu uliokwisha kwenye ligi hiyo, pia waliishia kufungwa ambao 2-0 na Mainz kwa kutoa pasi mbaya iliyomuangukia Sami Allagui wa Mainz aliyelifunga bao.

Na dakika nne kabla ya kumalizika muda Omer Toprak alijifunga mwenyewe alipojaribu kumzuia Marco Caliguiri.

Timu mgeni FC Augsburg katika mechi ya kwanza ya timu hiyo kwenye bundesliga, ilifanikiwa kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Freiburg.

Hertha Berlin iliyorudi kwenye ligi hiyo baada ya kuwa katika divisheni ya pili kwa msimu mmoja, ilifungwa 1-0 nyumbani na Nuremberg.

Awamu ya kwanza ilikosa uchangamfu na timu zote zilishindwa kutoa nafasi za kufunga kufikia muda wa mapumziko. Hali ilikuwa sawa katika awamu ya pili lakini kunako dakika 80 Nuremberg kupitia mchezaji wake mpya Tomas Pekhart ilifunga bao la pekee. Licha ya kushabikiwa na umati wa watu 60,00, Hertha Berlin ilishindwa kulisawazisha bao hilo na kuishia kuuanza msimu kwa kufungwa.

Bundesliga 1. Spieltag 2011/2012 VfB Stuttgart - FC Schalke 04
Picha: dapd

Stuttgart na Wolfsburg ndio timu zinazoongoza katika orodha ya ligi mpaka sasa baada ya kuzifunga Schalke 04 na FC Cologne 3-0 kila mmoja katika mechi zao za ufunguzi.

Cologne ilikamilisha mechi ikiwa na wachezaji 10 baada ya Milivoje Novakovic kutolewa uwanjani.

Katika mechi nyengine mwishoni mwa juma, Hanover 96 iliifunga Hoffeinheim 2-1, wakati Werder Bremen iliifunga Kaisersalutern mabao 2-0 nyumbani.

Hannover ilipata mkwaju wa penalti kunako nusu saa ya mchezo huo wakati Schlaudraff alipoangushwa na Mohammed Abdellaoue hakufanya kosa.

Na sasa Hertha Berlin inakabiliana na Nuremberg siku ya Jumamosi wakati Bayer Leverkusen inakaribishwa na Mainz siku ya Jumapili siku sawa ambapo Bayern Munich inaonana tena na Borussia Monchengladbach.

Kibarua kwa wachezaji Uingereza

Kwengineko katika kandanda ya Uingereza, wachezaji wa kiafrika waliomo kwenye timu hizo, wanajitahidi kuonyesha kustahili kwao kuzichezea timu hizo kama vile Chelsea, wakati msimu mpya wa ligi ya Uingereza ikianza.

Champions League FC Chelsea Spartak Moskau
Didier Drogbawa timu ya ChelseaPicha: AP

Mchezaji kama Didier Drogba na wenziwe wa Kiafrika wanaelekea kuuanza msimu mpya Uingereza wakiwa wamejitahidi kumhakikishia kocha mpya Andre Villas Boas kuwa wanastahili kuwa katika miaka ya usoni ya timu hiyo.

Kocha wa Chelsea ameahidi kutoa nafasi kwa wachezaji kuonyesha umahiri wao na hili huenda likawafurahisha wachezaji kama Drogba, Salomon Kalou, John Obi Mikel na Michael Essien.

Kitu kinachompa sifa kocha huyo mpya mwenye umri wa miaka 33 sawa na Drogba, ni kujiamini kwake jambo linaloashiria kuwa huenda asisite kuwaondoa wachezaji wa msimu kama Drogba.

Iwapo atasalia na mfumo wake wa 4-3-3, basi patakuwa na nafasi ya mchezaji moja kati ya Drogba au Fernando Torres aliyenunuliwa kwa pauni milioni 50 kuwa katika kiungo cha ushambulizi.

Hatahivyo raia huyo wa Côte d'Ivoire ana hakika ataishinda nafasi hiyo na amshawishi pia Villas Boas amuongezee mkataba wake unaomalizika mwezi Juni.

André Villas-Boas
Andre Villas-BoasPicha: dapd

Hali hii pia inawakabili wachezaji Mikel, raia wa Nigeria anayecheza kiungo cha kati, Mfungaji Kalou wa Côte d'Ivoire, na mchezaji wa kiungo cha kati, raia wa Ghana, Essien, wote wakiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wao kwenye timu hiyo ya Uingereza.

Mpaka sasa Mikel anatarajiwa kutimiza uwezo ulioifanya Chelsea iishinde Manchester United katika kumsajili huku naye Kalou hajawahi kuishikilia nafasi katika kikosi cha kwanza.

Essien kwa upande wake atakuwa nje kwa miezi sita inayokuja akiuguza maumivu ya goti baada ya kufanyiwa upasuaji ikiwa ni maumivu ya tatu makuu ya goti lake katika kipindi chake cha kucheza mpira kikazi.

Kwengineko mambo yanaonekana kumng'aria raia mwenza wa Drogba, anayetoka Côte d 'Ivoire, Gervinho katika timu ya Arsenal.

Kocha Arsene Wenger ameeleza kuwa mchezaji huyo aliyeiongoza timu ya Lille ya Ufaransa kuchukuwa taji la nchi hiyo, ni ongezeko zuri kwa Arsenal na huenda akaichukuwa nafasi ya Robin Van Persie. Wenger ameeleza kuwa anatangamana vizuri na wachezaji wenzake katika timu hiyo ya washikilia mizinga.

Arsene Wenger
Arsene WengerPicha: picture-alliance/ dpa

Yaya Toure, nyota wa Manchester City katika mashindano ya kombe la FA baada ya kufunga mabao katika nusu fainali na fainali pia msimu uliokwisha, anasisiitiza kuwa timu yake ipo tayari kuuchukuwa ubingwa kutoka timu jirani pinzani Manchester united.

Anasisitiza kuwa ni muhimu kutoa ujumbe kuanzia mwanzo, utakaodhihirisha kuwa Manchester City wamewasili na hawaendi kokote.

Wakati huo huo wachezaji Peter Odemwingie wa Nigeria na Asamoah Gyan wa Ghana wote wananuia kudhihirisha kuwa umahiri wao msimu uliokwisha ulikuwa sio wa bahati nasibu.

Mambo ni kangaja huenda yakaja! Msema kweli atajulikana uwanjani.

Mechi za kirafiki Afrika

Mipambano kati ya timu ya taifa ya Nigeria na Ghana ndio angazio kuu la mipambano ya kirafiki ya takriban wiki 14 yanayozijumuisha timu za Afrika katika kujitayarisha kwa michuano ya kufuzu mwakani ya kombe la taifa bingwa barani Afrika yatakayofanyika mwezi ujao.

Nusu ya timu za taifa za Afrika 52, zinazoshiriki zitashuka uwanjani Watford Uingereza hadi Msumbiji zikiwemo timu 7 kati ya 10 za juu kwenye orodha ya FIFA.

Afrika kusini inaikaribisha Burkina Faso, Senegal inaonana na Morocco mjini Dakar. Tunisia inakabiliana na Mali ambayo inawakosa wachezaji wake nyota, huku nayo Côte D'Ivoire ikipambana na Israel mjini Geneva.

Timu ambazo zinakosekana kwenye orodha ya mechi ni mabingwa wa Afrika wanaokosa mkufunzi Misri, timu ya Algeria inayojipanga upya chini ya ukufunzi mpya wa Mbosnia, Vahid Halihodzic, na Cameroon iliyoamua kwenda kwenye kambi ya mafunzo nchini Ufaransa.

Mipambano ya kirafiki kwa mara nyingi hukumbwa na wachezaji kujitoa dakika za miwsho kutokana na maumivu, na tayari mchezaji wa Afrika kusini wa kiungo cha kati ambaye pia ni kapteni, Steven Pienaar atakosekana huku mchezaji wa Nigeria aliyeitwa, Osaze Odemwingie amechelewa kufanyiwa ukaguzi wa afya.

Samuel Eto'o wa Cameroon, Michael Essien pia wanaouguza maumivu na Didier Drogbawa Côte D'Ivoire na Asamoah Gyan wa Ghana ndiyo wanaotazamiwa kuwa vivutio vikuu vya mechi hizo za Afrika.

Fussball Champions League Inter Mailand gegen Schalke 04 Samuel Eto'o
Samuel Eto'oPicha: AP

Wachezaji wengine kama kipa wa Ghana, Adam Kwarasey, mchezaji wa kiungo cha kati, Albert Adomah wanatambua kuwa michuano ya kirafiki hutoa nafasi za ajira za kimataifa.

Timu ya Senegal inatarajia kumpata mchezaji mzaliwa wa Ufaransa, Mbaye Niang alichezee taifa hilo la Afrika, walikozaliwa wazaazi wake.

Mali inaitembelea Tunisia, ikiwa inawakosa wachezaji wake nyota kama Paris st.Germain, Mohammed Sissoko anayeshughulika zaidi na kandanda ya kilabu, na Mahamadou Diarra aliyesimamishwa kucheza, huku mchezaji wa kiungo cha kati wa Barcelona, Seydou Keita akisemekana kukataa ombi la kuichezea timu hiyo ya Afrika.

Mwandishi: Maryam Dodo Abdalla
Mhariri:Abdul-Rahman