Musharaf ashitakiwa kwa mauaji ya Bhutto
20 Agosti 2013Mashitaka dhidi ya Pervez Musharaf yamesomwa mbele yake mahakamani mjini Rawalpindi, huku kukiwa na ulinzi mkali. Anatuhumiwa kuuawa, kushiriki katika njama za mauaji, na kusaidia katika mauaji. Hata hivyo, wakili wa Musharaf, Syeda Afsham Adil amesema tuhuma hizo hazina msingi, na wala hawana wasiwasi wowote kuhusiana na kesi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa mtu ambaye alikuwa mkuu wa jeshi nchini Pakistan kushitakiwa mahakamani kwa kosa lolote. Ingawa si wengi wanaoamini kuwa upo ushahidi wa kutosha kumweka hatiani Musharaf, hatua hiyo ya mahakama inatuma ujumbe mzito kwamba nguvu za jeshi la nchi hiyo zimepungua mnamo miaka ya hivi karibuni.
Ripoti yasema Bhutto hakupatiwa ulinzi wa kutosha
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2010 kuhusu kuuawa kwa Bi Benazir Bhutto ilisema kuwa kifo chake kingeweza kuzuiwa, na iliilaumu serikali iliyokuwa ikiongozwa na Musharaf kushindwa kumpatia kiongozi huyo wa upinzani ulinzi wa kutosha.
Benazir Bhutto ambaye alichaguliwa mara mbili kuwa waziri mkuu wa Pakistan aliuawa tarehe 27 Desemba mwaka 2007, katika shambulizi la kujitoa mhanga. Yeye alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa taifa la kiislamu.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Pakistan Imtiaz Gul amesema kesi dhidi ya Musharaf itachukua muda mrefu, na itakuwa vigumu sana kwa mahakama kuweza kuthibitisha kuwa alihusika kwa vyovyote vile katika mauaji dhidi ya Bhuto. ''Tunachokishuhudia ni mashitaka yenye malengo ya kisiasa, ambayo hatimaye yataambulia patupu'', amesema mchambuzi huyo.
Uwezekano wa makubaliano
Mashitaka haya ya leo hayajanyamazisha minong'ono iliyopo, juu ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya chini chini, ambayo yanaweza kumruhusu Musharaf kuondoka nchini Pakistan bila kwenda gerezani.
Hilo halitakuwa jambo jipya kwa Pakistan, kwani hata waziri mkuu wa sasa Nawaz Sharif aliwahi kuhukumiwa kifungo cha maisha baada ya kuangushwa na Musharaf mwaka 1999, lakini akaruhusiwa kuondoka na kwenda kuishi uhamishoni nchini Saudi Arabia, ambako alitoka na kushinda uchaguzi wa mwezi Mei uliomweka madarakani.
Mchambuzi Imtiaz Gul amesema wapo watu wenye ushawishi kutoka nchi za nje kama vile Saudi Arabia, Marekani na Uingereza, ambao wanaweza kufanya usuluhishi na kupata makubaliano kuhusu Musharaf kama yale ya Nawaz Sharif.
Mwezi Novemba mwaka 2011, mahakama hiyo hiyo ya Rawalpindi iliwafungulia mashitaka maafisa wawili wa polisi pamoja na watu wengine watano wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la Taliban kuhusu mauaji ya Bi Bhutto, lakini hadi sasa hakuna kesi iliyokwishaendeshwa dhidi ya watuhumiwa hao.
Hadi sasa hakuna upande wowote uliojitokeza na kudai kuhusika na mauaji ya Benazir Bhutto, Serikali ya Musharaf ilimshutumu kiongozi wa Taliban nchini Pakistan kwa wakati huo Baitullah Mehsud kupanga mauaji hayo. Huyo naye aliuawa na ndege za Marekani zisizoendeshwa na rubani mwaka 2009.
Hii siyo kesi pekee inamkabili Pervez Musharaf tangu kurudi nchini Pakistan akitokea ukimbizini mwezi Machi mwaka huu. Nakabiliwa pia na mashitaka ya uhaini na kukiuka katiba, ambayo adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/AP
Mhariri:Josephat Charo