Muungano tawala Ethiopia kuunda chama kimoja cha siasa
22 Novemba 2019Vyama vitatu kati ya vinne vinavyounda muungano wa Demokrasia ya Mapinduzi ya Watu wa Ethiopia, EPRDF, vimekubaliana kuunda chama kimoja cha kitaifa kuelekea uchaguzi utakaofanyika mwezi Mei mwakani.
Chama hicho kipya kitaitwa Prosperity Party. Hata hivyo chama kimoja cha Tigrayan People's Liberation Front (TPLF) kilisusia makubaliano hayo na kusema hatua ya kuundwa chama kimoja cha kitaifa ni kama imeharakishwa na siyo ya kidemokrasia.
Kulingana na msemaji wake, Fekadu Tessema, viongozi wa vyama vitatu vinavyounda muungano waliidhinisha mpango wa chama kimoja. "Uamuzi wa makubaliano uliopitishwa wa vyama kuungana ni hatua muhimu ya kutumia nguvu zetu kufanya kazi kwa maono ya pamoja," alisema waziri mkuu Abiy Ahmed kwenye taarifa yake.
Zoezi hilo limedhihirisha ni jinsi gani taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, lilivyogawika juu ya msukumo wa waziri mkuu Abiy wa kuiunganisha nchi na makundi tofauti ya kikabila ambayo yanatafuta uhuru zaidi.
Abiy ana matumaini kwamba mageuzi yake ya haraka yanaweza kuwashawishi wapiga kura ambao wametengwa kwa miongo kadhaa ya dhuluma za muungano tawala kabla ya uchaguzi wa mwakani.
Muungano wa Demokrasia ya Mapinduzi ya Watu wa Ethiopia EPRDF, ulianzisha mfumo wa kisiasa baada ya kutwaa madaraka mwaka 1991, ambayo yanatoa uhuru muhimu kwa mikoa tisa ya kikabila inayodhibiti kodi za ndani, elimu na majeshi yake ya usalama.
Jamii ya watu wa Sidama walipiga kura ya maoni wiki hii ya kuamua iwapo waunde jimbo jipya la watu wa Sidama. Matokeo yake yanasubiriwa kwa hamu na yanaweza kuchochea makundi mengine ya kikabila kutaka uhuru zaidi.
Tume ya uchaguzi ya Ethiopia inatarajia kutangaza matokeo ya kura hiyo ya maoni siku ya Jumamosi. Hadi sasa Ethiopia imegawika katika majimbo tisa ambayo yana uhuru nusu huku kura ya maoni ya Sidama ikiweka uwezekano wa kuwepo na jimbo la 10.
Kura hiyo ya maoni iliyofanyika Jumatano wiki hii ilimalizika kwa amani. Waziri mMuu Abiy aliwashukuru watu wa Sidama kwa kupiga kura kwa amani. Dhamira ya kutaka uhuru zaidi kulichochea ghasia za mwezi Julai na kusababisha watu kadhaa kuuwawa na hivyo serikali ikauweka mkoa wa kusini chini ya udhibiti wa wanajeshi na polisi wa shirikisho.