Mvua kubwa yasababisha maafa nchini Japan
10 Julai 2023Mtu mmoja amepoteza maisha huku mamia kwa maelfu wakihimizwa kuondoka kwenye makaazi yao katika eneo la Kusini Magharibi mwa Japan siku ya Jumatatu, wakati idara za utabiri wa hali ya hewa zikitoa tahadhari ya mvua kubwa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo.
Mvua kubwa iliyonyesha baada ya wiki moja ya mvua mfululizo imesababisha kingo za mito kuvunjika na maporomoko ya udongo ikiwa ni pamoja na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 77. Nyumba ya mwanamke huyo iliteketea usiku kucha katika eneo la Saga, idara ya zimamoto ya eneo hilo imelieleza shirika la habari la AFP. Mumewe alipona na kupelekwa hospitalini.
Maafisa wanasema mwanamke mwengine anahofiwa kufa baada ya kuonekana mara ya mwisho akining'inia katika gari lililokuwa limesombwa kwenye maji ya mafuriko katika mkoa jirani wa Oita.
Watu wengine tisa hawajulikani walipo katika mkasa huo wa maporomoko ya ardhi katika mikoa ya Fukuoka na Oita, ambapo zaidi ya watu 420,000 walipewa tahadhari ya hali ya juu ya kuondoka, iliyosema: "Maisha yako yako hatarini, unahitaji kuchukua hatua mara moja."
Takriban watu milioni mbili zaidi katika maeneo ya Fukuoka, Hiroshima, Saga, Yamaguchi na Oita nao pia wamepewa tahadhari ya kuondoka kwenye makaazi yao hatarishi.
Soma pia: Mataifa kadhaa ya Asia yakumbwa na mvua kubwa
Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japani JMA ilisema mvua hiyo kubwa ilihatarisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo ya Fukuoka na Oita. Mkuu wa kitengo cha utabiri wa hali ya hewa kutoka mamlaka ya JMA Satoshi Sugimoto aliwaambia waandishi wa habari, "hii ndiyo mvua kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa."
Ofisi ya waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida imesema kikosi kazi kimeundwa kushughulikia athari za mvua hizo.
Maporomoko ya ardhi ni hatari hasa nchini Japani wakati wa mvua kubwa kwa sababu nyumba mara nyingi hujengwa kwenye maeneo tambarare chini ya vilima katika nchi hiyo ya milima.
Mnamo mwaka 2021, mvua ilisababisha maporomoko ya ardhi katika mji wa mapumziko wa Atami na kuua watu 27. Mwaka 2018, mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliua zaidi ya watu 200 magharibi mwa Japani wakati wa msimu wa mvua.
Chanzo: AFP