1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Mwaka 2024 unakaribia kuwa wenye joto zaidi kuwahi kutokea

11 Aprili 2024

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa mawimbi makubwa ya joto katika eneo la mashariki mwa bara la Asia na Pasifiki yanaweza kuwaweka mamilioni ya watoto hatarini na kutoa wito wa kutafuta mbinu za kuwalinda watoto

https://p.dw.com/p/4efWU
Bangladesch Dhaka Hitzewelle
Mwaka 2024 unakaribia kuwa mwaka wenye joto kali zaidi kuwahi kutokeaPicha: Syed Mahamudur Rahman/NurPhoto/picture alliance

Ripoti ya Umoja wa mataifa imesema kuwa mawimbi makubwa ya joto katika eneo la mashariki mwa bara la Asia na Pasifiki yanaweza kuwaweka mamilioni ya watoto hatarini. Ripoti hiyo iliyotolewa mapema leo imetoa mwito pia wa kuchukuliwa hatua ili kuwalinda watoto walio hatarini kutokana na hali ya joto inayoongezeka.

Wachunguzi wa kimataifa wameonya kuwa mwaka wa 2024 unakaribia kuweka rekodi ya mwaka wenye joto kali zaidi, hali hiyo ikielezwa kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la uzalishaji wa gesi chafu.

Soma zaidi: UNICEF: Ukeketaji wanawake waathiri wanawake milioni 230

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Watoto UNICEF,zaidi ya watoto milioni 243 kote bara la Asia na Pasifiki wanakadiriwa kuathirika zaidi na joto na kuwaweka katika hatari ya magonjwa yanayotokana  na joto na hata kutokea kwa vifo.

2024
Watoto katika mataifa ya bara la Asia na Pasifiki wapo katika hatari kubwa ya kukumbana na magonjwa yanayotokana na joto kaliPicha: Fabio Teixeira/Anadolu/picture alliance

Kwa sasa, nchi kadhaa katika eneo hilo zinapitia katika hali ya joto kali, takwimu zilizorekodiwa karibuni zikionyesha nyuzi joto sasa zinafikia 40 katika kiwango cha Celsius.

Wataalam: Joto linaweza kuongezeka zaidi

Watabiri wa hali ya hewa wa eneo hilo wanatabiri kuwa hali hiyo ya joto kali inaweza kuongezeka kwa kasi zaidi katika wiki zijazo.

Baadhi ya shule nchini Ufilipino zimesimamisha masomo kufuatia kuongezeka kwa joto kali, ripoti hiyo ikiongeza kuwa katika baadhi ya maeneo ya Ufilipino kiwango cha joto kinaweza kufikia nyuzi joto 42 au 43 cha Celsius.

Soma zaidi. Watoto 68,000 Nepal wahitaji msaada

Nchini Thailand nyuzi joto 43.5 zilirekodiwa katika jimbo la kaskazini la Mae Hong Son mapema wiki hii ikiwa ni nyuzi chache tu kuifikia rekodi ya nyuzi joto 44.6.

Watoto
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watoto bilioni mbili wanatarajiwa kuathirika kutokana na joto kali ifikapo mwaka 2050Picha: Tercio Teixeira/AFP

Kwa mujibu wa wizara ya afya nchini Thailand, takriban watu 40 hufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na joto kila mwaka.

Mwezi Februari mwaka huu, nchi jirani ya Vietnam ilikumbana na wimbi la joto katika eneo la kusini mwa nchi ambapo joto lilifikia hadi nyuzi joto 38, rekodi ya juu kabisa kuwahi kurekodiwa katika eneo hilo.

Debora Comini, Mkurugenzi wa Ofisi ya UNICEF ya Kanda ya Asia Mashariki na Pasifiki amesema, watoto wako katika hatari zaidi kuliko watu wazima kwani hawana uwezo wa kudhibiti joto la mwili wao.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watoto bilioni mbili wanatarajiwa kuathirika kutokana na joto kali ifikapo mwaka 2050.