1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Watoto huzaliwa katika mazingira hatari huko Gaza

19 Januari 2024

Umoja wa Mataifa umesema maelfu ya watoto huzaliwa katika mazingira "yasiyoelezeka" huko Gaza tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na kundi la Hamas. Baadhi ya wagonjwa hufanyiwa operesheni bila ganzi.

https://p.dw.com/p/4bTXa
Rafah | Mtoto mchanga aliyehamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Gaza
Mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati huko Gaza akipewa maziwa huko Rafah baada ya kuhamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa iliyoshambuliwa na vikosi vya Israel: Novemba 19,2023Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Mtaalam wa masuala ya Mawasiliano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Tess Ingram, ambaye amehitimisha hivi karibuni ziara yake katika Ukanda wa Gaza, anasema alishuhudia wanawake sita wajawazito wakivuja damu hadi kufa wakati wakifanyiwa upasuaji wa dharura.

UNICEF inasema karibu watoto 20,000 wamezaliwa katikati mwa vita hivyo vilivyodumu siku 105 huku baadhi ya wanawake wajawazito wakifanyiwa upasuaji bila ganzi na wengine wakilazimika kuondoka hospitalini masaa matatu tu baada ya operesheni hiyo kutokana na wingi wa wagonjwa.

Soma pia: UN: Hali katika hospitali za Gaza ni mbaya mno

Akizungumza kwa njia ya video na waandishi wa habari waliopo mjini Geneva, Uswisi, Ingram amesema akiwa nchini Oman kuwa wastani wa mtoto mmoja huzaliwa kila baada ya dakika 10 huku vita hivyo vikiendelea huku akitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kimataifa ili kukomesha hali hiyo.

Msaada wa kiutu wa Umoja wa Mataifa huko Gaza
Shehena ya msaada wa kibinaadamu wa Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF ulioandaliwa na Wafanyakazi wa UNRWA kwa ajili ya hospitali huko Deir Al-Bala katika Ukanda wa Gaza: 25.10.2023Picha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

" Kuwa mama inapaswa kuwa wakati wa kusherehekea. Lakini huko Gaza, kila mtoto anapozaliwa, ni kama anazaliwa katika jehannam. Ubinadamu hautakiwi kuruhusu hali hii isiyo ya kawaida iendelee. Akina mama na watoto wachanga wanahitaji usitishwaji mapigano kwa sababu za kibinadamu."

Israel yaendeleza mashambulizi kusini mwa Gaza

Hadi sasa zaidi ya watu 24,700 wamearifiwa kuuawa na wengine zaidi ya 62,000 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na kundi la Hamas.

Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi kadhaa za Magharibi kama kundi la kigaidi.

Hivi karibuni jeshi la Israel lilisema idadi kamili ya wanamgambo wa Kipalestina waliouawa katika  Ukanda wa Gaza  imefikia 9,000 huku ikiwapoteza pia wanajeshi wake 194. Vita hivyo vilichochewa na mauaji mabaya zaidi katika historia ya Israel, yaliotekelezwa na wapiganaji wa Hamas Oktoba 7, 2023 ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuawa.

Gaza- Uharibifu uliotokana na mashambulizi ya Israel
Uharibifu uliotokana na mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: DW

Urusi imeitolea wito Hamas kuwaachilia mateka wote, ikisema hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza imefikia viwango "vya kutisha". Wito huo ulitolewa wakati wa mazungumzo mjini Moscow na afisa mwandamizi wa Hamas Musa Abu Marzouk.

Soma pia: Israel yatofautiana na Marekani kuhusu kuundwa taifa la Palestina

Lakini pia, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu katika eneo la Palestina amesema leo Ijumaa kuna uwezekano kuwa maelfu ya  wanaume wa Gaza wamezuiliwa na wanajeshi wa Israel  tangu kuibuka vita hivyo na kwamba wengi wao huenda wanakabiliwa na vitendo vya mateso.

Katika harakati za kidiplomasia, Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watafanya mfululizo wa mikutano siku ya Jumatatu ambapo watakutana na wenzao kutoka Israel, Mamlaka ya Palestina na mataifa kadhaa ya Kiarabu ili kujadili vita vya huko Gaza na matarajio ya kupatikana suluhu ya amani.

(Vyanzo: Mashirika)