Mwanajeshi wa Israel akamatwa kwa kumpiga risasi Mpalestina
25 Machi 2016Kwa mujibu wa jeshi la Israel, tukio hilo limetokea kwenye mji wa Hebron, katika Ukingo wa Magharibi, baada ya Wapalestina wawili kudaiwa walihusika kumchoma kisu na kumjeruhi mwanajeshi wa Israel. Jeshi hilo limesema wanajeshi kisha waliwauawa kwa kuwapiga risasi Wapalestina hao.
Video hiyo iliyochukuliwa na Mpalestina anayefanya kazi ya kujitolea katika shirika la haki za binaadamu la Israel, B'T selem, imemuonyesha mwanajeshi huyo akimpiga risasi kichwani Mpalestina ambaye tayari alikuwa amejeruhiwa.
Jeshi la Israel limesema Fatah a-Sharif na Ramzi al-Qasrawi, wote wakiwa na umri wa miaka 21, walipigwa risasi wakati walipomrukia na kumvamia mwanajeshi wa Israel na kisha kumchoma kisu na kumjeruhi. Mwanajeshi huyo alikuwa akilinda katika kizuizi kilichoko ndani ya mji wa Hebron.
Msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Peter Lerner amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba hilo ni tukio baya ambalo ni kinyume na sheria za vikosi vya ulinzi vya Israel na dhidi ya kile kinachotarajiwa na wanajeshi wa Israel pamoja na makamanda wao.
Idara ya ulinzi ya Israel imekiri kutokea kwa mauaji hayo na imeanzisha uchunguzi wa kina wa tukio hilo, ambalo limeripotiwa pia na makamanda wa jeshi. Kwa mujibu wa idara hiyo, tayari mwanajeshi huyo amesimamishwa kazi.
Tukio hilo litashughulikiwa kwa umakini mkubwa
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Moshe Yalon, ameahidi kuwa tukio hilo litashughulikiwa kwa umakini mkubwa. Akizungumza katika video iliyosambazwa kwa waandishi wa habari, Yalon amesema uchunguzi kuhusu tukio hilo ulishaanza hata kabla ya video hiyo kusambazwa kwenye mitandao.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema wanajeshi wanapaswa kujizuia wenyewe. Katika taarifa yake, Netanyahu amesema jeshi linatarajia wanajeshi wake waishi kwa utulivu kwa mujibu wa sheria za kazi.
Video hiyo inatishia kuchochea zaidi mvutano ulipo, huku kukiwa na mfululizo wa ghasia kati ya Waisrael na Wapalestina, ambazo ziliibuka mwezi Oktoba mwaka uliopita. Kwa mujibu wa maafisa wa Israel, wengi wa Wapalestina waliouawa walikuwa wameshika visu, bunduki au walishiriki kwenye matukio ya kuwagonga watu kwa magari.
Waziri wa Afya wa Palestina, Jawad Awwad ameliita tukio hilo kama 'uhalifu wa kivita' akisema hata kabla ya mauaji hayo, madaktari katika eneo na tukio hawakumtibu mwanaume huyo aliyekuwa amejeruhiwa, na badala yake walikuwa wakimtibu tu mwanajeshi wa Israel aliyejeruhiwa.
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu likiwemo, Amnesty International wamekosoa vikali mauaji hayo, wakisema siyo ya haki na mhusika anapaswa kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita.Vikosi vya Israel vimeshutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi katika baadhi ya matukio, madai ambayo hata hivyo wameyakanusha.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,AP,DPA
Mhariri: Yusuf Saumu