Mwendesha mashtaka mauaji ya Rais wa Haiti aachishwa kazi
15 Septemba 2021Frantz Louis Juste, mwendesha mashtaka aliyesimamia kesi iliyohusisha vifo vya zaidi ya watoto 12 walioteketea katika kituo cha watoto yatima mjini Port-au-Prince mwaka jana, sasa ndiye mwendesha mashtaka mpya katika kesi hiyo.
Wiki iliyopita, mwendesha mashtaka katika kesi hiyo Bed-Ford Claude alisema, rekodi za simu zinaonyesha kwamba mtu anayeshukiwa kuwa mpangaji mkuu wa mauaji ya Moise, aliwasiliana na Waziri Mkuu Henry usiku ambao uhalifu huo ulifanyika. Kulingana na Claude, walizungumza mara mbili kwa kipindi cha dakika saba kila mara.
Haki haiwezi kuzuiwa na wahusika watafunguliwa mashtaka na kuadhibiwa
Mshukiwa huyo Joseph Baido ambaye alikuwa afisa katika wizara ya sheria na ambaye Henry amekuwa akimtetea, anadaiwa kutoroka na hajulikani alipo kwa sasa.
Mwishoni mwa wiki, waziri mkuu huyo alikuwa amezungumzia suala la haki kuhusiana na mauaji ya Moise.
"Vitendo vya kuleta mkanganyiko na kuzuia haki haviwezi kukubalika. Wahusika wa kweli na waliopanga mauaji ya Rais Jovenel Moise watafunguliwa mashtaka na wataadhibiwa kwa vitendo vyao."
Waziri Mkuu wa Haiti Henry, ambaye ni daktari wa upasuaji aliteuliwa namarehemu Moise kama waziri mkuu siku chache kabla kuuwawa kwake na anataka kuleta maelewano kati ya mirengo mbalimbali ya kisiasa. Ila madai ya kuhusika kwake katika mauaji ya Moise, sasa yameifunika hiyo azma yake ya kuleta maelewano ya kisiasa nchini humo.
Polisi waliagizwa kumuongezea ulinzi mwendesha mashtaka
Haijawa wazi iwapo kuondolewa kwa Claude kutakuwa na athari yoyote katika kesi hiyo ila wachambuzi nchini humo wanasema hawatarajii mengi kuhusiana na kesi hiyo kubadilika kwasababu uchunguzi upo mikoni mwa jaji.
Hapo Jumatatu, Waziri wa sheria nchini humo Rockfeller Vincent aliiagiza polisi ya Haiti kumuongezea ulinzi Claude kwasababu alikuwa amepokea vitisho kwa kipindi cha siku tano.
Fauka ya hayo, makarani wa korti wanaripotiwa kwenda mafichoni baada ya kupokea vitisho vya kuuwawa iwapo hawatobadilisha baadhi ya majina na taarifa katika ripoti zao. Mbali na hayo, jaji mmoja aliyepewa jukumu la kusimamia uchunguzi katika kesi hiyo alijiuzulu mwezi uliopita kwa kile alichosema ni sababu za kibinafsi lakini mmoja wa wasaidizi wake alifariki kwa njia ya utata.
Vyanzo: AP/Reuters