Mzozo wa Sahel waendelea kufukuta
31 Januari 2024Ikizingatiwa kwamba Umoja huo hautaki kushirikiana na vikosi vya kijeshi vya Urusi vinavyoendelea kutanua wigo wake.
Akizungumza kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi huko mjini Brussels, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borel amesema uamuzi wa mataifa yanayoongozwa na tawala za kijeshi: Mali, Burkina Faso na Niger, kujiondoa kutoka kwa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, umeibua utata zaidi katika suala la uwepo wa Umoja wa Ulaya katika eneo la Sahel.
Soma pia:Umoja wa Afrika wasema "umefadhishwa" na kujiondoa Niger, Mali na burkina Fasso ndani ya ECOWAS
Borel ameongeza kusema kwamba Urusi tayari ilikuwa na nguvu nchini Mali na inaweza pia hivi karibuni kuingia Niger na Burkina Faso. Ujumbe wa Umoja wa Ulaya una hadi Mei 24 kuamua iwapo utaendelea kubaki nchini Mali. Ameongeza kusema kwamba bado ujumbe wa Umoja huo ungali nchini Mali na bila shaka hautaki kushirikiana na vikosi vya Urusi vya Africa Corps.
Rais wa mpito wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore, amesema kwamba hakuna raia wa Urusi ambaye kwa sasa ametumwa nchini humo kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali lakini hakupinga uwezekano wa vikosi vya Urusi kupelekwa katika siku zijazo.
Soma pia: Nigeria yazikosoa Mali, Niger na Burkina Faso kujitoa ECOWAS
Matarajio ya Urusi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, amesema anatarajia mvutano ndani ya jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi unaweza kutatuliwa:
"Tunatumai kuwa matatizo yaliyojitokeza katika uhusiano kati ya wanachama wa ECOWASyanaweza kutatuliwa kwa mazungumzo sawa na ya kuheshimiana. Kwa upande wetu, tulisisitiza kuwa Urusi iko tayari kuendelea kuchangia juhudi za kuleta utulivu katika eneo la Sahara-Sahel na maeneo mengine barani Afrika."
Waziri mkuu wa Burkina Faso, Appolinaire Joachimson Kyelem de Tambela, amesema kujiondoa kwa Burkina Faso, Mali na Niger kutoka jumuiya ya ECOWAS ni "uamuzi uliozingatiwa kwa makini" kujibu matumaini ya "mamlaka ya kujitawala".
Ikumbukwe kwamba Burkina Faso, Mali na Niger walikuwa wanachama waanzilishi wa jumuiya ya ECOWAS mwaka 1975, lakini umoja huo ulizisimamisha uwanachama nchi zote tatu kufuatia mapinduzi ya kijeshi.
Umoja wa Afrika hapo jana ulisema umesikitishwa na uamuzi wa serikali hizo za kijeshi. Rais wa Halmashauri wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alitoa wito kwa viongozi wa kanda kuzidisha mazungumzo kati ya uongozi wa ECOWAS na nchi hizo tatu ambazo zilishutumu jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi kwa kuwa tishio kwa uhuru wao.
//Reuters, AFP