1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yazidi kuimiminia mabomu Libya, Uturuki yamkana Gaddafi

4 Julai 2011

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imezidisha mashambulizi yake dhidi ya Libya kwa kuishambulia miji kadhaa ya nchi hiyo usiku wa kuamkia leo (04.07.2011), huku Uturuki ikitangaza kuacha kufanya kazi na serikali ya Gaddafi.

https://p.dw.com/p/11oc9
Sehemu ya maafa ya NATO mjini Janzour, Libya
Sehemu ya maafa ya NATO mjini Janzour, LibyaPicha: AP

Kwa mujibu wa televishini ya serikali ya nchi hiyo, Jamahariyya, ambayo imenukuu vyanzo vya kijeshi, ndege za NATO zililenga kituo cha usalama kilichopo mji wa Bani. Kituo hicho kipo umbali wa kilometa 200 kusini mashariki mwa Tripoli, kikiwa bado kipo chini ya himaya ya utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.

Kuna taarifa kwamba hivi karibuni serikali ya Libya iliwakusanya baadhi ya wanawake na kuwapeleka katika kituo hicho na kuwapa mafunzo ya kijeshi.

Vile vile, mashambulizi ya NATO yalilenga bandari na vituo vya ukaguzi katika eneo la ukanda wa eneo la pwani wa Zuwara, lililopo umbali wa kilometa 125 magharibi mwa mji mkuu wa Tripoli.

Zuwara ni moja kati ya bandari sita nchini Libya ambayo hapo Juni 2011 Umoja wa Ulaya uliiwekea vikwazo. Mwezi uliopita maafisa 34 kutoka mji wa Zuwara waliasi upande wa Gaddafi na kujiunga na upinzani.

Uturuki yamuacha mkono Gaddafi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu (katikati) akizungumza mjini Benghazi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu (katikati) akizungumza mjini BenghaziPicha: AP

Katika hatua nyingine, Uturuki imekatisha uhusiano wake wa kibalozi na serikali ya Gaddafi na kumwita balozi wake nyumbani. Hatua hiyo inadaiwa kufuatia ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu katika makao makuu wa waasi mjini Benghazi hapo jana.

Katika ziara hiyo, Davutoglu ameahidi kutoa msaada dola milioni 200 za Kimarekani kama msaada kwa Baraza la Mpito la Libya, ambacho ni chombo cha kisiasa cha waasi wa Libya.

Pamoja na kueleza kwamba Uturuki imelitambua Baraza hilo kama chombo kinachowakilisha wananchi, Davtoglu pia alisema kwamba wakati umefika kwa Gaddafi kuondoka madarakani.

Waasi 'wamualika' Gaddafi kuendelea kuishi Libya

Mkuu wa Baraza la Mpito la Libya, Mustafa Abdul Jalil
Mkuu wa Baraza la Mpito la Libya, Mustafa Abdul JalilPicha: picture alliance/dpa

Kwa upande wao, waasi wamesema kwamba wanamkaribisha Kanali Gaddafi kuendelea kuishi nchini Libya, ikiwa atakubali kujiuzulu kwa hiari yake. Kiongozi wa waasi, Mustafa Abdel-Jalil, amesema hatua hiyo ina lengo la kurejesha amani nchini humo.

Hata hivyo, Abdel-Jalil amesema kwamba masharti ya 'mualiko' huo wa Gaddafi kustaafia ndani ya nchi yake, ni kwa kiongozi huyo kwanza kujiuzulu na kuamuru majeshi yake kurudi makambini.

"Halafu anaweza kuchagua kama anataka kwenda kuishi uhamishoni au abakie nchini Libya." Amesema Abdel-Jalil.

Kwa upande wake, mtoto Gaddafi, Saif al-Islam, alikiambia kituo cha televishini cha Ufaransa (TFI) kwamba kumshinikza baba yake kuondoka madarakani ni dhihaka, na kwamba jambo hilo kamwe halitofanyika, bali watapigana mpaka hatua ya mwisho.

Vita vyaendelea

Wakati huo huo, mapambano makali kati ya waasi na majeshi ya serikali yanaripotiwa kuendelea katika maeneo kadhaa ya Libya. Msemaji wa waasi aliyeko Misrata amesema kuwa wapiganaji wao wawili wameuwawa katika mapigano kati ya vikosi vyao na majeshi ya serikali, wakati wakifanya jitahada za kuyarudisha nyuma majeshi hayo.

Vuguvugu la kutumia silaha kumuondoa Gaddafi, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 42 sasa, lilianza katikati ya mwezi Februari, pale wapinzani walipoyabadili maandamano yao kuwa mapigano ya kutumia silaha, baada ya serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za kuwakandamiza.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman