1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uhuru wa vyombo vya habariUjerumani

Navalnaya apokea tuzo ya DW ya uhuru wa kujieleza 2024

6 Juni 2024

Yulia Navalnaya, mjane wa mpinzani wa Kremlin Alexei Nalany, amepokea tuzo ya Deutsche Welle ya uhuru wa kujielezea mwaka huu 2024.

https://p.dw.com/p/4gjJO
Tuzo ya Deutsche Welle ya uhuru wa kujielezea mwaka 2024
Tuzo ya Deutsche Welle ya uhuru wa kujielezea mwaka 2024Picha: DW

Wakfu wa marehemu mume wake Navalny wa kupambana na ufisadi pia ulitambuliwa katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Berlin jana Jumatano kutokana na mapambano yake dhidi ya jaribio la serikali ya Urusi kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. 

Katika hotuba aliyoitoa wakati akipokea tuzo hiyo, Navalnaya amesema wakfu huo utaendelea na kazi yake licha ya kifo cha mumewe ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Soma pia: Juhudi za kukuza uhuru wa habari zapungua duniani 

Mjane huyo wa Navalny amewahimiza wanasiasa wa mataifa ya Magharibi kusema ukweli hata katika "nyakati ngumu.”

"Nimefurahi kupokea tuzo hii ya kifahari, tuzo ya uhuru wa kujieleza ya Deutsche Welle. Ni muhimu pia kuelezea mchango wa wakfu wa kupambana na ufisadi ambao mume wangu Alexei Navalny, aliuanzisha miaka 13 iliyopita. Ni muhimu kwa sababu, katika miaka yote hiyo, uhuru wa kujieleza umekuwa silaha na nguzo muhimu zaidi iliyoko hai.”

Alexei Navalny, alikufa katika mazingira tatanishi kwenye gereza la Siberia mapema mwaka huu.

Yulia Navalnaya, mjane wa Alexei Navalny, amesimama kwenye foleni akiwa na wapiga kura wengine katika kituo cha kupigia kura karibu na ubalozi wa Urusi mjini Berlin
Yulia Navalnaya, mjane wa Alexei Navalny, amesimama kwenye foleni akiwa na wapiga kura wengine katika kituo cha kupigia kura karibu na ubalozi wa Urusi mjini BerlinPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Navalnaya ameweka wazi kuwa Putin ndio aliomuua mumewe japo hakufanikiwa kuzima ndoto na mawazo yake. Ametahadharisha juu ya habari potofu zinazoenezwa na Urusi na mipango ya hujuma ndani ya Umoja wa Ulaya kuelekea uchaguzi wa bunge la ulaya wiki hii.

Navalnaya ambaye amechukua kijiti cha upinzani kutoka kwa mumewe, ameeleza kuwa Putin anajaribu kulazimisha ajenda yake na kwamba mara kwa mara anafanikiwa.

Soma pia: Mjane wa Navalny aahidi kuendeleza kazi yake 

Hata hivyo ameahidi kuendelea na mapambano na anaamini kuwa hatimaye uhuru wa kujieleza utaibuka na ushindi dhidi ya sumu ya propaganda.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner aliyekuwepo kwenye hafla hiyo mjini Berlin, alimkabidhi Navalnaya tuzo hiyo ya Deutsche Welle ya uhuru wa kujielezea.

Navalnaya atajwa kama mwanamke mpambanaji

Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner akihojiwa na DW wakati wa hafla ya tuzo ya Deutsche Welle ya uhuru wa kujielezea mwaka huu 2024
Waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner akihojiwa na DW wakati wa hafla ya tuzo ya Deutsche Welle ya uhuru wa kujielezea mwaka huu 2024Picha: Ronka Oberhammer/DW

Lindner amemwagia sifa Navalnaya na kumtaja kama "mshirika imara” wa Navalny na mpambanaji wa mawazo huru.

"Licha ya hali kutotabirika, hatupaswi kukata tamaa na kufahamu kuwa wakati uko upande wetu. Ukweli ni kwamba muda wa Putin kuendelea kusalia madarakani utafikia kikomo siku moja, kitu kinachotupa matumaini kwamba wakati utakuja ambapo Urusi itakuwa tayari kwa demokrasia.

Waziri huyo wa fedha wa Ujerumani amesema Rais Vladimir Putin anakalia kuti kavu.

Soma pia:  EU yatafakari vikwazo vipya kufuatia kifo cha Navalny

Hafla hiyo ya mjini Berlin ilikuwa toleo la kumi la tuzo ya uhuru wa kujielezea ambayo inalenga kuangazia pandashuka na vizuizi zinavyovikabili vyombo vya habari kote duniani.

Kibali cha kuliruhusu shirika la habari la Ujerumani Deutsche Welle kupeperusha matangazo au maudhui yake mitandaoni nchini Urusi kilifutwa na mamlaka nchini humo mnamo mwaka 2022.

Ofisi ya Deutsche Welle iliyokuwa mjini Moscow ilifungwa na kuhamishwa hadi mji mkuu wa Latvia wa Riga.