1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Navalny atarajiwa kuzikwa kusini mwa jiji la Moscow

Saleh Mwanamilongo
1 Machi 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny aliyefariki dunia gerezani wiki mbili zilizopita, anatarajiwa kuzikwa Ijumaa mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/4d42x
Mazishi ya Navalny yamepangwa kufanyika siku ya Ijumaa huko Maryino, viungani mwa jiji la Moscow
Mazishi ya Navalny yamepangwa kufanyika siku ya Ijumaa huko Maryino, viungani mwa jiji la MoscowPicha: Dmitri Lovetsky/AP Photo/picture alliance

Jamaa na wafuasi wa Alexei Navalny watauaga mwili wa kiongozi huyo wa upinzani katika mazishi yatakayofanyika kusini mashariki mwa jiji la Moscow. Ibada ya mazishi imetarajiwa kufanyika katika hali ya sintofahamu kufuatia mvutano baina ya familia na mamlaka juu ya kutolewa kwa mwili wa Navalny baada ya kifo chake katika mazingira ya kutatanisha.

Familia na wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani wanasema makanisa kadhaa huko Moscow yalikataa kuendesha ibada ya mazishi kabla ya timu ya Navalny kupata ruhusa kutoka kwa mmojaya kanisa katika wilaya ya Maryino, ambapo Navalny aliishi hapo awali kabla ya kupewa sumu mwaka 2020 na kuletwa hapa nchini Ujerumani kwa matibabu.

Vitisho vya serikali ya Urusi

Urusi yatishia kuwakamata watu watakaojitokeza kwenyre mazishi ya Navalny
Urusi yatishia kuwakamata watu watakaojitokeza kwenyre mazishi ya NavalnyPicha: Alexander Nemenov/AFP/Getty Images

Kanisa la Maria Mama wa Mungu, ambalo lilikubali kufanya ibada hiyo, hata hivyo halikutoa tangazo lolote kwenye mitandao yake ya kijamii. Polisi siku ya Alhamisi walionekana wakiweka vizuizi vya kudhibiti umati kanisani huko. Ibada ya wafu itafuatiwa na mazishi katika makaburi ya Borisovskoye, ambapo polisi pia walionekana wakipiga doria jana Alhamisi.

Hata hivyo, waombolezaji wengi walikuwa wakisubiri karibu na kanisa la Mother of God, ambapo ibada imepangwa kuanza saa nane mchana, saa za Moscow.

Mama wa Navalny, Lyudmila Navalnaya, alitumia siku nane kujaribu kupata ruksa za mamlaka ili kutoa mwili huo kufuatia kifo chake mnamo Februari 16. Maafisa awali walisema hawakuweza kurejesha mwili kwa familia kwa sababu walihitaji kufanya uchunguzi wa baada ya maiti. Navalnaya alitoa mwito kwa Rais Vladimir Putin kuachilia mwili wa mwanaye ili aweze kumzika kwa heshima.

Kitendawili kwa familia ya Navalny

Alexei Navalny alikufa mnamo 16 Februari katika gereza la Urusi la Arctic Circle na alikuwa amefungwa jela miaka mitatu kwa makosa ya uwongo
Alexei Navalny alikufa mnamo 16 Februari katika gereza la Urusi la Arctic Circle na alikuwa amefungwa jela miaka mitatu kwa makosa ya uwongoPicha: Evgeny Feldman/AP Photo/picture alliance

Mjane wake, Yulia Navalnaya, aliwalaumu Putin na Meya wa Moscow Sergei Sobyanin kujaribu kuzuia umma kuhudhuria mazishi. Putin, ambaye hajawahi kutamka jina la Navalny hadharani, hajazungumza chochote kuhusu kifo hicho.

Mamlaka ya Urusi haijatangaza sababu ya kifo cha Navalny. Alexei Navalny mwenye umri wa miaka 47 alikuwa mpinzani mkuu wa Putin ambaye alipinga ufisadi na kuitisha maandamano makubwa

kote nchini Urusi. Viongozi wengi wa nchi za magharibi walilaani kifo cha mpinzani huyo wa Urusi.

Haikuweza kufahamika mara moja ni nani kati ya familia ya Navalny au washirika wake atahudhuria mazishi, pamoja na washirika wake wengi walio uhamishoni nje ya nchi kwa sababu ya hofu ya mashtaka nchini Urusi. Timu ya Navalny ilisema mazishi yake yataonyeshwa moja kwa moja kupitia chaneli ya YouTube ya Navalny.

Vyanzo: AP, AFP