1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawaz Sharif ajiandaa kurejea ulingoni Pakistan

13 Mei 2013

Mshindi wa uchaguzi nchini Pakistan Nawaz Sharif, yuko katika mazungumzo ya kuunda serikali, huku matatizo ya kiuchumi na uasi wa kutumia silaha vikionekana kuwa ndiyo changamato zake kuu mbili.

https://p.dw.com/p/18WfU
Nawaz Sharif akizungumza katika ngome yake mjini Lahore
Nawaz Sharif akizungumza katika ngome yake mjini LahorePicha: picture alliance/AP Photo

Matokeo rasmi katika uchaguzi huo wa Jumamosi bado kutangazwa, lakini chama cha Sharif cha Pakistan Muslim League-Nawaz, (PML-N) kina uhakika wa kupata ushindi. Matokeo hayo yanaonyesha kurudi tena kwa Sharif mwenye umri wa miaka 63, ambae aliondolewa ofisini kama waziri mkuu mwaka 1999 kupitia mapinduzi ya kijeshi, na kisha kukaa jela na uhamishoni kwa miaka kadhaa.

Kiongozi wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf PTI, Imran Khan.
Kiongozi wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf PTI, Imran Khan.Picha: Getty Images

Sartaj Aziz, Afisa mwandamizi wa chama cha PML-N amesema Sharif alifanya mazungumzo siku ya Jumapili na baadhi ya wabunge wa kujitegemea, kwa lengo la kushirikiana nao katika uundwaji wa serikali mpya. Sharif alikuwa waziri mkuu wa Pakistan kuanzia mwaka 1990 hadi 1993 alipoondolewa kufuatu ugomvi na rais na jeshi, na baadae kuanzia mwaka 1997 hadi 1999, alipopinduliwa na jeshi.

Baada ya kupinduliwa mara mbili huko nyuma

Taswira iliyotolewa na vituo vya televisheni ilionyesha kuwa hakuna chama ambacho kingepata ushindi wa moja kwa moja katika bunge la Pakistan lenye wajumbe 342. Lakini matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Sharif mpaka sasa kimepata viti 130, huku kile cha Pakistan Peopele's Party PPP, kikiwa na viti 33 na chama cha Tahreek-e-Insaf PTI kikiwa na viti 29. Nawazi Sharif atakuwa mtu wa kwanza kushika nafasi ya waziri mkuu kwa mara tatu nchini Pakistan, akitumai kuwa baada ya kupinduliwa na jeshi mara mbili, mara hii atafanikiwa kukamilisha muhula wake wa miaka mitano.

Ulikuwa ni ushindi wa kuridhisha wa chama cha Sharif dhidi ya chama cha PPP kilichoitawala Pakistan kwa miaka mitano iliyopita, ambacho kwa miongo kadhaa kimekuwa ndicho mbadala pekee katika mbio za uongozi wa nchi hiyo. Lakini uchaguzi huu umeibua nguvu mpya katika siasa za Pakistan - chama cha PTI, cha mchezaji maarufu wa Kriketi Imran Khan. Siku ya Jumapili, Khan alikubali kushindwa, lakini alisifu uhudhuriaji mkubwa wa wapiga kura katika uchaguzi huu, akiuita mwamko wa kisiasa.

"Tumesonga mbele sasa, mchakato wa kidemokrasia umesonga mbele. Lakini jambo kubwa kwangu ni kwamba chama cha Tareek-e-Insaf kimekuwa imara na tutatekeleza wajibu wetu kama chama cha upinzani," alisema Khan.

Wafuasi wa chama cha Nawaz Sharif cha PML-N wakishangilia wakati matokeo yakiendelea kutangazwa mjini Lahore.
Wafuasi wa chama cha Nawaz Sharif cha PML-N wakishangilia wakati matokeo yakiendelea kutangazwa mjini Lahore.Picha: Reuters

Sura mpya ya siasa za Pakistan

Na muhimu zaidi pengine, chama cha Imran Khan cha PTI kitabadilisha namna siasa za Pakistana zinavyoendeshwa. Chama hiki kimefanikiwa kuvutia idadi kubwa ya wapiga kura vijana, wakiwemo mamilioni ya wapiga kura wa mara ya kwanza. Katika kampeni iliyoanza mapema sana kabla ya uchaguzi huu, PTI iliweka ajenda ambayo msingi wake ulikuwa masuala muhimu kama vile uchumi na kupigana dhidi ya rushwa, na hivyo kuvunja mfumo uliojengwa kwa itikadi za kikabila, ambamo familia na makundi ya kimaslahi vilifanya chaguo za kisiasa badala ya watu binafsi.

Jambo moja ambalo halikubadilika katika uchaguzi huu, ni tatizo la vurugu za kisiasa, ambalo limegharimu maisha ya watu kadhaa wakati wa kampeni. Vurugu hizi zinasababishwa na itikadi kali ya dini ambayo ni changamoto kubwa zaidi inayoikabili serikali mpya.

Lakini katika wakati wa kutafakari kati ya kutolewa kwa matokeo na kuundwa kwa serikali mpya, jambo moja limedhihirika wazi. Kufikia tamati kwa mfumo wa utawala wa vyama viwili nchini Pakistan kunamaanisha kuwa sura ya siasa za nchi hiyo imebadilika.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga)dpae,ape
Mhariri: Daniel Gakuba