1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama waimarishwa katika uchaguzi wa Pakistan

MjahidA11 Mei 2013

Mamilioni ya raia wa Pakistan wanashiriki katika uchaguzi wa kihistoria utakaoonesha demokrasia katika kipindi cha mpito kwenye nchi inayomiliki silaha za nyuklia na nchi iliotawaliwa kijeshi kwa nusu ya historia yake.

https://p.dw.com/p/18W03
Maafisa wa Usalama Pakistan
Maafisa wa Usalama PakistanPicha: picture-alliance/dpa

Kundi la waasi la Taliban limeitaja demokrasia kuwa jambo ambalo haliendani na uislamu na wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara kwa vyama visivyoegemea misingi ya kidini na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200 katika mashambulizi yaliotajwa kuwa mabaya zaidi kwa wakati wa uchaguzi.

Hii imeongeza wasiwasi kwamba huenda kukafanyika mashambulizi katika vituo vya kupigia kura.

Vituo hivyo vilivyofunguliwa saa mbili kamili asubuhi vinatarajiwa kufungwa saa kumi na moja jioni kutoa nafasi kwa takriban wapiga kura milioni 86 wanaowachaguwa wabunge 342 katika bunge la Pakistan.

Raia wa Pakistan nje ya vituo vya kupiga kura
Raia wa Pakistan nje ya vituo vya kupiga kuraPicha: AP

Huku hayo yakiarifiwa usalama umeimarishwa nchini humo, zaidi ya maafisa wa polisi 600,000 wamesambazwa kote katika vituo 70,000 vya kupigia kura Pakistan.

Uchaguzi huu unatoa nafasi ya kwanza kabisa kwa utawala uliochaguliwa na raia kumaliza muda wake na kutoa nafasi kwa utawala mwengine kuingia madarakani kupitia uchaguzi. Pakistan imekumbwa na visa vitatu vya mapinduzi na kutawaliwa kijeshi mara nne.

Kibarua kigumu kiko kati ya Nawaz Sharif na Imran Khan

Kinyan'ganyiro kikali kiko kati ya waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif ambaye pia ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kati kulia wa (PML-N) na mchezaji bingwa wa mchezo wa Kriketi Imran Khan aliyeahidi mabadiliko nchini humo na kukomesha ufisadi iwapo atachaguliwa.

Mgombea mwingine ni Tehreek-e-Insaf wa chama cha (PTI) aliye na umri wa miaka 60 aliyeanguka siku ya Jumanne wakati alipokuwa katika harakati ya kampeni zake.

Waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa upinzani Nawaz Sharif
Waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa upinzani Nawaz SharifPicha: picture-alliance/ dpa

Hata hivyo kwa sasa Tehreek-e-Insaf yuko hospitalini na anakopokea matibabu baada ya kupata jeraha la uti wa mgongo na inasemekana kwamba hatoweza kupiga kura yake hii leo.

Chama tawala hakionekani kushamiri katika kampeni

Wakati huo huo Chama tawala kinachoondoka cha mrengo wa kati kushoto PPP kimekuwa na kampeni ambazo hazikuonekana kufua dafu sana kwa kuwa mwenyekiti wake Bilawal Bhutto Zardari, anaonekana kuwa mdogo sana katika kugombea na pia amekuwa akifichwa kufuatia vitisho vya waasi wa Taliban dhidi yake.

Chama hicho cha PPP kiliwapoteza viongozi wake wakuu muanzilishi wa chama hicho Zulfikar Ali Bhutto aliyenyongwa chini ya utawala wa kijeshi mwaka wa 1979 na mtoto wake Benazir Bhutto aliyeuwawa kwa kupigwa risasi katika shambulizi la kujitoa mhanga mwaka wa 2007.

Maswala muhimu ambayo utawala mpya unapaswa kuyashughulikia ni kuinua uchumi wa nchi hiyo, kutatua maswala ya kawi hali inayosababisha kukatika kwa umeme kwa zaidi ya saa 20, Juhudi inayoongozwa na Marekani ya kupambana na waasi wa itikadi kali za kiislamu, ufisadi na maendeleo ya Pakistan.

Mwenyekiti wa chama cha PPP Bilawal Bhutto Zardari
Mwenyekiti wa chama cha PPP Bilawal Bhutto ZardariPicha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo wanaharakati wengi ndani na nje ya Pakistan wanajiuliza iwapo wapiga kura watajitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo kutokana na vitisho vya waasi wa Taliban kushambulia vituo vya kupiga kura.

Awali msemaji wa kundi hilo Ehsanullah Ehsan aliwataka raia kususia uchaguzi wa leo ili kulinda maisha yao.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Caro Robi.