Nawaz Sharif arejea Pakistan baada ya miaka minne
22 Oktoba 2023Nawaz alirejea mjini Lahore siku ya Jumamosi (Oktoba 21) na kushiriki mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama chake cha Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari mwaka 2024.
Waziri mkuu huyo wa zamani aliwaambia wafuasi wake kwamba anakutana nao kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, lakini bado ana mapenzi na chama chake na wafuasi wake hawajamsaliti na hajawasaliti.
Soma zaidi: Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif arejea nyumbani
Pakistan inapitia changamoto ya usalama, kudorora kwa uchumi wa taifa hilo na mgogoro wa kisiasa wakati ikijitayarisha kuandaa uchaguzi huo mkuu, huku mpinzani mkubwa wa Sharif, Imran Khan, akiendelea kufungwa jela kwa makosa ya ufisadi.
Sharif aliyefungwa jela kwa makosa sawa na hayo, aliachiwa kutoka jela kwa dhamana mwaka 2019 kwa lengo la kupata matibabu mjini London kwa wiki sita, lakini baadaye aliamua kutorejea Pakistan kumaliza kifungo chake.