Netanyahu na Biden wajadili kuhusu mazungumzo ya Doha
13 Januari 2025Makubaliano hayo pia yanalenga kuachiliwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas katika ukanda wa Gaza na Wapalestina walioko katika magereza ya Israel.
Netanyahu amemwambia Biden kuhusu jukumu aliloipa timu inayoshiriki mazungumzo hayo mjini Doha ili kuendeleza juhudi za kuachiliwa huru mateka, na pia amewashkuru Biden na Rais mteule Donald Trump kwa msaada wao katika kufanikisha hilo.
Soma pia: Israel yaua dazeni kadhaa Gaza katikati mwa juhudi za kumaliza vita
Ikulu ya Marekani imeeleza kwamba, Biden na Netanyahu walijadili juu ya mazungumzo yanayoendelea mjini Doha na kuachiliwa kwa mateka kwa kuzingatia mpango wa kusitisha mapigano uliowasilishwa na Biden mnamo mwezi Mei mwaka uliopita.
Kulingana na taarifa ya Ikulu ya Marekani, viongozi hao wawili walizungumza pia kuhusu mazingira ya kikanda yaliyobadilika kufuatia hatua ya kusitishwa mapigano nchini Lebanon, kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria na kudhoofika kwa ushawishi wa Iran katika eneo hilo.