Upinzani Myanmar waelezea hofu ya kupokonywa ushindi
10 Novemba 2015Chama cha NLD kinasema kina wasiwasi kwamba utawala wa kijeshi unapanga kuyachafua matokeo halisi ya uchaguzi, siku mbili baada ya wananchi wa Myanmar kupiga kura zao.
Ingawa kiongozi wa chama hicho, Aung San Suu Kyi, hakutaja tuhuma hizo kwenye mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la BBC, ambapo alisema serikali inayoungwa mkono na jeshi imeahidi kuheshimu matokeo, msemaji wa NLD, Win Htien, aliwaambia waandishi wa habari kwamba "haingii akilini kuwa bado Tume ya Uchaguzi inaendelea kutoa matokeo vipande vipande hadi sasa."
Kufikia leo (Jumanne 10 Novemba), Tume hiyo ilikuwa imetoa matokeo ya viti 83 tu kati ya viti 664 vya bunge, ambapo kwenye viti hivyo, NLD ilishinda 74 na vinne kwenda kwa chama tawala. Kwa mujibu wa matokeo yaliyokusanywa na NLD yenyewe, chama hicho kinachoongozwa na mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel kimeshinda viti 154 kati ya viti 164 kwenye majimbo 14 ya nchi hiyo, huku Tume ya Uchaguzi ikitangaza kuwa chama hicho kimeshinda viti 11 kati ya 15 kwenye mikoa minne.
Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa wasifu upigaji kura
Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walisema kuwa upigaji kura kwa kiwango kikubwa ulikuwa mzuri zaidi kuliko hata ilivyokuwa imetazamiwa hapo awali, ingawa bado kuna mageuzi zaidi yanayohitajika kwenye mfumo wa chaguzi katika taifa hilo la kusini mwa Asia.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini Yangon, mkuu wa ujumbe wa waangalizi hao, Alexandar Graf Lambsdorff, aliwapongeza raia wa Myanmar kwa kupiga kura kwa amani Jumapili iliyopita.
"Kwa kadiri ambavyo mchakato wa upigaji kura na vituo vya kura unahusika, basi asilimia 95 ya waangalizi wetu wanasema ulikuwa mzuri au mzuri sana, na hiyo ni asilimia kubwa sana. Mchakato huu ulikwenda vyema zaidi kuliko wengi walivyotazamia hapo awali. Hata hivyo, ni jambo lisilo shaka kuwa mengi zaidi yanahitajika kubadilishwa ili kuhakikisha uchaguzi wa siku zijazo unakuwa wa haki kwelikweli", alisema.
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ambaye amewapongeza pia watu wa Myanmar kwa uvumilivu wao, heshima na hamasa kubwa wakati wakishiriki uchaguzi wa juzi. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, aliwaambia waandishi wa habari jijini New York kuwa wadau wa ndani na nje ya nchi hiyo walitimiza wajibu wao ipasavyo kwenye uchaguzi huu.
"Waangalizi kwenye uchaguzi huu, wawe wa ndani au wa nje, wamekishuhudia kipindi hiki cha kihistoria. Katibu Mkuu anafahamu kwamba matokeo yameanza kukusanywa na anawapongeza wadau wote nchini Myanmar kwa kudumisha moyo wa heshima, utulivu na umoja kwenye mchakato mzima wa kukamilisha uchaguzi huu."
Jumla ya wapigakura milioni 33 na nusu halali walimiminika kwenye vituo zaidi ya 46,000 siku ya Jumapili, ambapo wagombea 6,038 kutoka vyama 91 vya kisiasa na wengine 310 waliosimama kama wagombea huru walikuwa wanawania takribani viti 1,000 vya ubunge.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman