Obama apendekeza Hagel kwenye ulinzi
7 Januari 2013Obama ameamua kwamba seneta huyo wa zamani kutoka Republican mwenye umri wa miaka 66, ndiye atakayekuwa mrithi wa Leon Panetta na anatarajiwa kutangaza uteuzi huo hii leo, kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa kutoka serikalini na shirika la habari la AFP, na hivyo kuthibitisha ripoti za vyombo vya habari vya Marekani.
Obama pia anatarajiwa kumtangaza atakaechukua nafasi ya David Petraeus katika uongozi wa CIA, wakati kaimu mkurugenzi Michael Morell na mshauri wa masuala ya ugaidi John Brennan wakipewa nafasi kubwa kwa mujibu wa kituo cha Televisheni cha Marekani cha CNN.
Pamoja na ukweli kwamba Hagel anatoka chama cha Republican, amekuwa akilaumiwa na vigogo wa chama hicho kwa kuonyesha uadui dhidi ya Israel na asiye na ufahamu juu ya Iran hivyo kufanya mchakato wa uteuzi kuwa mgumu.
Upinzani dhidi ya Hagel
Seneta Mitch McConnel kutoka Republican alimsifu Hagel wakati alipoamua kuachia kiti chake cha Nebraska mwaka 2009 kwa ''sauti ya wazi na sifa juu ya usalama wa taifa na sera za kigeni'', lakini sauti yake ilikuwa tofauti siku ya Jumapili. ''Ni lazima apewa nafasi ya kusikilizwa kama alivyo mteuliwa yoyote na atakuwa',' McConnel alikiambia kituo cha ABC .
Katika mahojiano na CNN, seneta kiongozi wa Republican Linsey Graham hakuwa na aibu ya kumshambulia moja kwa moja, akisema Hagel atakuwa ni '' Waziri mwenye upinzani juu ya hali ya Israel katika historia ya taifa letu.''
Akaongeza kuwa ''siyo tu kwamba amesema unatakiwa moja kwa moja kujadiliana na Iran, vikwazo havitaweza kufanya kazi, kwamba Israel pia inapaswa kujadiliana na Hamas, shirika na kundi la kigaidi ambalo limerusha maroketi Israel. Yeye pia alikuwa ni mmoja wa maseneta 12 ambao walikataa kusaini barua kwa Umoja wa Ulaya kujaribu kuwataja Hezbollah kama shirika la ugaidi.'' Alisema Graham.
Seneta mwingine wa Republican, John Cornyn wa Texas, amesema atapinga uteuzi huo akisema itakuwa ni "ujumbe mbaya zaidi tutakaoupeleka kwa rafiki yetu Israel na washirika wengine huko Mashariki ya Kati.''
Hagel anajulikana kwa ukali wake na mtu mwenye kujitegemea anayesema bila kificho. Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na gazeti la historia la Vietnam, alikanusha kwamba yeye si mfuasi wa kupinga vita.
''Ninaamini katika kutumia nguvu, lakini baada ya kufanya maamuzi kwa uangalifu. Nitafanya lolote niwezalo kuepuka vita''
Kama atadhibitishwa na seneti kama waziri wa ulinzi, Hagel atapaswa kusimamia kupunguzwa kwa matumizi ya kijeshi wakati juhudi za Marekani za kuhitimisha vita nchini Afghanstan zikimalizika na kujiandaa kwa matukio mabaya nchini Iran na Syria.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu