Obasanjo aonya kuhusu mazungumzo Ethiopia
15 Novemba 2021Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumapili, Obasanjo, rais wa zamani wa Nigeria amesema ana matumaini kwamba makubaliano ya pamoja kuelekea katika kupatikana suluhisho la amani katika mzozo huo yanaweza kufikiwa. Matamshi hayo ameyatoa baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na viongozi wa kundi la waasi la Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF.
Obasanjo ambaye anaongoza juhudi za kimataifa za kujaribu kuumaliza mzozo unaoendelea nchini Ethiopia ambayo tayari umeyagharimu maisha ya maelfu ya watu na kuwalazimisha wengine milioni mbili kuyakimbia makaazi yao, aliondoka Ethiopia siku ya Alhamisi. Obasanjo hata hivyo ameonya kuwa mazungumzo kama hayo hayawezi kufanikiwa bila ya pande zinazohasimiana kusitisha mapigano mara moja.
Hofu yatanda
Hayo yanaelezwa huku hofu ikiongezeka kwamba waasi wanaelekea kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na kusababisha hali ya sintofahamu katika shughuli za kidiplomasia. Obasanjo ameutaka uongozi wa kila upande kusitisha operesheni za kijeshi, hatua itakayoruhusu fursa ya mazungumzo kuendelea.
Mjumbe maalum wa Marekani Jeffrey Feltman pia aliizuru Ethiopia wiki iliyopita kwa ajili ya mazungumzo. Obasanjo ameitoa kauli hiyo siku chache kabla ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken kwenye nchi tatu za Afrika. Blinken anaunga mkono juhudi za Obasanjo za kuwa mpatanishi na ametishia kuweka vikwazo kwa serikali ya Abiy na kundi la TPLF, hadi hapo pande hizo mbili zitakapoendelea na mazungumzo.
Wakati huo huo, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye pia anashiriki katika juhudi za upatanishi za kikanda, jana alikutana na Waziri Mkuu Abiy mjini Addis Ababa katika ziara ya siku moja ambayo haikutangazwa awali. Kenyatta pia alikutana na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde na viongozi wa vyama vya kisiasa.
Ofisi ya rais wa Kenya haikutoa maelezo zaidi kuhusu kile kilichojadiliwa mjini Addis Ababa kati ya Kenyatta na viongozi wa Ethiopia, lakini gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa kiongozi huyo alikwenda Ethiopia katika juhudi za kutafuta amanina kujadiliana kuhusu masuala ya kikanda.
Hata hivyo, vyombo vya habari vya Ethiopia vimeielezea ziara ya Kenyatta mjini Addis Ababa kama ya kibinafsi. Novemba 3, Rais Kenyatta aliwataka viongozi wa pande zinazohasimiana kaskazini mwa Ethiopia kutafuta njia ya kusitisha mapigano mara moja na kushiriki katika meza ya mazungumzo.
Umoja wa Mataifa watoa msaada wa dharura
Huku hayo yakijiri, Umoja wa Mataifa umesema umetoa fedha za dharura kwa ajili ya misaada ya kiutu kwa lengo ya kuokoa maisha na ulinzi wa raia waliokwama katika mzozo unaoendelea Ethiopia. Mkuu wa ofisi inayoshughulika na misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths amesema ametoa jumla ya dola milioni 40 zinazotarajiwa kuongeza operesheni za dharura kwenye jimbo la Tigray na maeneo mengine ya kaskazini mwa Ethiopia ambako kuna mzozo.
Siku ya Alhamisi Ethiopia iliweka masharti ya uwezekano wa kufanyika mazungumzo na waasi, ikiwemo kusitishwa mashambulizi, TPLF kuondoka kwenye maeneo ya Amhara na Afar na kutambua uhalali wa serikali. Kundi la TPLF kwa upande wake linataka msaada kupelekwa kwenye jimbo la Tigray, ambako mzozo ulizuka mwaka uliopita. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hadi sasa hakuna msaada wowote ulioingizwa kwa njia ya barabara tangu Oktoba 18 na malori 364 yamekwama Afar yakisubiru kibali.
(AFP, AP)