1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oxfam: Utajiri wa mabilionea uliongezeka mno 2024

20 Januari 2025

Shirika la kimataifa la kupambana na umasikini Oxfam limesema siku ya Jumatatu kuwa utajiri wa mabilionea uliongezeka mara tatu zaidi mwaka uliopita wa 2024.

https://p.dw.com/p/4pNws
Jarida la Forbes la mwaka 2010 likiwaangazia matajiri wakubwa duniani
Jarida la Forbes la mwaka 2010 likiwaangazia matajiri wakubwa dunianiPicha: Xinhua/imago images

Shirika hilo la Oxfam limesema utajiri wa mabilionea ulikua kwa dola trilioni 2 mwaka jana, ikiwa ni sawa na takriban dola bilioni 5.7 kwa siku, ikiwa ni mara tatu zaidi kuliko mwaka 2023. 

Idadi ya mabilionea iliongezeka kwa kuibuka mabilionea 204 na hivyo kupelekea idadi hiyo kufikia hadi 2,769, huku watu 10 ambao ni matajiri zaidi duniani wakishuhudia utajiri wao ukiongezeka kwa wastani dola milioni 100 kwa siku. Oxfam ilitumia chapisho la mwezi Novemba la jarida la Forbes linalowaangazia mabilionea wakubwa duniani.

Soma pia:Watu 62 wanamiliki nusu ya utajiri wa dunia 

Utafiti huu wa Oxfam unaipa uzito kauli iliyotolewa wiki iliyopita na rais wa Marekani anayemaliza muda wake Joe Biden ambaye alitahadharisha kuhusu "mkusanyiko hatari wa mamlaka mikononi mwa matajiri wachache." Ripoti ya kundi hilo yenye jina la "Takers Not Makers,"ikizingatia takwimu za Benki ya Dunia, inaeleza pia kuwa idadi ya watu maskini wanaoishi na chini ya dola 6.85 kwa siku haijapungua tangu mwaka 1990.

Kundi la matajiri lazusha wasiwasi

Bilionea Elon Musk (kushoto) akiwa na Rais wa Marekani Donald Trump
Bilionea Elon Musk (kushoto) akiwa na Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Mitabh Behar, Mkurugenzi mtendaji wa  Oxfam International, amesema katika mahojiano kuwa kuingia madarakani kwa Trump akisaidiwa na mshauri wake Elon Musk kunatoa picha ya kwamba kundi la matajiri wakubwa duniani ndiyo wanashikilia usukani wa uongozi. Ameongeza kuwa hilo halimhusu mtu mmoja lakini ni mfumo wa kiuchumi ulioundwa ambapo sasa mabilionea wanaweza kuunda sera za kiuchumi na kijamii ambazo hatimaye huwanufaisha zaidi.

Sambamba na wito wa Biden wa kuwataka mabilionea waanze kulipa kodi na ushuru unaofaa, shirika la Oxfam limetoa wito kwa serikali za mataifa mbalimbali kuwatoza ushuru zaidi matajiri ili kupunguza hali ya ukosefu wa usawa na kukabiliana na utajiri uliokithiri.

Soma pia: Matajiri waomba kutozwa kodi

Shirika hilo limetoa wito wa kuchukuliwa hatua kama vile kuondoa ukiritimba, kudhibiti malipo ya wakurugenzi watendaji, na kuhakisha mashirika yanawalipa wafanyakazi mishahara stahiki.

Mwaka 2024, wawekezaji wengi walipata faida kubwa, hasa kutoka kwenye makampuni makubwa ya teknolojia, faharisi za soko la hisa, bei ya dhahabu na hata sarafu za mtandaoni. Oxfam imeendelea kuwa kwa wastani nchi zenye kipato cha chini na cha kati hutumia karibu nusu ya matumizi ya bajeti zao za kitaifa ili kulipa madeni.

Ripoti yaambatana na kongamano la Davos

Bango ka kongamano la kimataifa la kiuchumi la Davos, Uswisi
Bango ka kongamano la kimataifa la kiuchumi la Davos, UswisiPicha: World Economic Forum Annual Meet/Avalon/IMAGO

Ripoti hiyo ya Oxfam imetolewa wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la kiuchumi litakaloanza leo hadi Ijumaa huko Davos, shirika la Oxfam International katika tathmini yake ya hivi punde kuhusu hali ya ukosefu wa usawa duniani, limetabiri kuwa angalau matrilionea watano wataibuka katika muongo ujao.

Watu wapatao 3,000 wakiwemo wadau wa biashara, wasomi, viongozi wa serikali, na wawakilishi wa vikundi vya kiraia wanatarajia kuhudhuria kongamano hilo la kila mwaka katika mji wenye milima wa Davos nchini Uswisi.

Soma pia: Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19

Rais mteule wa Marekani Donald Trump, ambaye alihudhuria mara mbili kongamano la Davos wakati wa muhula wake wa  kwanza, anatarajiwa mara hii kushiriki kwa njia ya video siku ya Alhamisi. Kwa muda mrefu, Trump aliyekula kiapo Jumatatu amekuwa akitetea suala la kujilimbikizia utajiri huku akimteua bilionea Elon Musk kama mshauri wake.

Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, waandamanaji kadhaa wameshuhudiwa huko Davos wakidai uwepo hatua za kiuchumi, kuwatoza ushuru matajiri na kushinikiza madai mengine yanayotetea usawa wa kijamii.

(Chanzo: AP)