Pakistan inawasaka wahusika wa shambulizi la kigaidi
28 Machi 2016Msemaji wa jeshi la Pakistan, Asim Bajwa amesema msako huo umeanza ili kuwafikisha katika mkono wa sheria waliohusika na mauaji ya watu wasio na hatia. Naibu Inspekta Mkuu wa polisi, Haider Ashraf, ameiambia DW kwamba vikosi vya usalama vimeimarisha ulinzi wa usalama kuzunguka Lahore, mji mkuu wa jimbo la Punjab, kwa sababu wako katika hali ya vita.
''Tunatumia mashirika maalum kama vile ya kupambana na ugaidi, kufanya uchunguzi. Kuna masuala kadhaa yanayotuelekeza kwa mshambuliaji aliyejitoa mhanga na watu walio nyuma ya shambulizi hili,'' Inspekta Ashraf
Mshambuliaji aliyejitoa muhanga alijiripua jana kwenye mji huo katika bustani ya mapumziko ya Gulshan-i-Iqbal, ambako Wakristo wengi walikuwa wamekusanyika kusherehekea sikukuu ya Pasaka. Wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto.
Kundi la Jamaat-ul-Ahrar lililojitenga na Taliban, limekiri kuhusika na shambulizi hilo, likisema lilikuwa likiwalenga hasa Wakristo. Msemaji wa kundi hilo, Ehsanullah Ehsan, amesema shambulizi hilo linatoa ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif, kwamba wameingia Lahore na kamwe hawezi kuwazuia. Pakistan ni taifa lenye Waislamu wengi, lakini idadi ya Wakristo ni zaidi ya milioni mbili.
Serikali yatangaza siku tatu za maombolezo
Serikali ya jimbo la Punjab leo imetangaza siku tatu za maombolezo, huku bendera ya taifa ikipepea nusu mlingoti na taasisi zote za elimu kwenye mji wa Lahore, zimefungwa. Shambulizi katika jimbo hilo, sio la kawaida kwa sababu ni moja kati ya majimbo tajiri na yenye utulivu.
Pakistan imekuwa ikijitahidi kupambana na uasi wa Taliban pamoja na ghasia za kidini. Wakati makundi ya Taliban Pakistan na Jamaat-ul-Ahrar yakifanya mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya usalama na serikali, pia mara nyingi yamekuwa yakiwalenga Wakristo na Waislamu wa madhehebu ya Kishia.
Viongozi wengi wakiwemo viongozi wa Kikristo pamoja na Waziri Mkuu Nawaz Sharif, wamelaani vikali shambulizi hilo. Nawaz leo amewatembelea majeruhi wa shambulizi hilo waliolazwa hospitalini pamoja na familia zao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amelaani vikali shambulizi hilo akisema ni ugaidi unaotisha na ametaka wahusika waadhibiwe haraka kwa mujibu wa sheria. Ban ambaye ametoa salamu zake za rambirambi kwa wahanga na familia zao na kuonyesha mshikamano, ameitolea wito serikali ya Pakistan kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa kila mmoja, zikiwemo jamii za watu wachache wanaoishi nchini humo.
Naye mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai, amelaani shambulizi hilo huku akiitaka Pakistan na dunia nzima kuungana. Katika mtandao wake wa Twitter, Malala ameandika kwamba maisha ya kila mtu yana thamani na lazima yaheshimiwe na kulindwa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTR,AFP,DPA
Mhariri: Josephat Charo