1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVatican

Papa Francis: Kuna haja ya kurekebisha mustakabali wa kanisa

4 Oktoba 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesema kuna haja ya kurekebisha mustakabali wa kanisa hilo ili liwe mahala pa kumkaribisha kila mmoja, na sio kikwazo kinachosababishwa na hofu na itikadi.

https://p.dw.com/p/4X6KV
Italien | Welt-Bischofssynode in Rom
Picha: Andrew Medichini/AP Photo/picture alliance

Matamshi hayo ameyatoa Jumatano wakati akifungua Sinodi ya XVI ya Maaskofu Ulimwenguni iliyotanguliwa kwa Ibada ya Misa takatifu katika Viwanja vya Mtakatifu Peter, mjini Vatican. Miongoni mwa ajenda zitakazotawala katika Sinodi hiyo ni pamoja na jukumu la wanawake na mtazamo wa kanisa kuhusu watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Waumini wa Kikatoliki wanaopenda maendeleo wana matumaini kuwa Sinodi hiyo itachangia wanawake zaidi katika nafasi za uongozi, huku wahafidhina wakionya kuwa inaweza kuligawa kanisa.

Papa akiri kuhusu mgawanyiko uliopo

Katika mahubiri yake, Papa Francis amekiri kuhusu mgawanyiko wa kiitikadi uliopo, lakini amewasihi waumini kuuweka pembeni na badala yake wamsikilize Roho Mtakatifu. ''Hatupo hapa kufanya mkutano wa bunge au mpangi wa matengenezo. Sinodi sio bunge. Mhusika mkuu ni yeye, Roho Mtakatifu. Tuko hapa kutembea pamoja na Yesu," alisisitiza Papa Francis.

Papa Francis amekumbushia kuhusu somo wake, Mtakatifu Francisco wa Asizi, ambaye sikukuu yake inaadhimishwa Jumatano, ambaye pia alikabiliwa na migawanyiko na mivutano katika maisha yake na alifanikiwa kuijibu kwa sala, upendo, unyenyekevu na umoja, pale alipoambiwa: ''Nenda ukalijenge upya kanisa langu.'' Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amewataka waumini kufanya sawa na alichokifanya Mtakatifu Francisco wa Asizi.

Italien | Welt-Bischofssynode in Rom
Maaskofu wanaohudhuria Sinodi ya XVi ya Maaskofu mjini VaticanPicha: Andrew Medichini/AP Photo/picture alliance

Kumekuwepo wa wito wa kuwainua wanawake zaidi na kuwajumuisha katika ngazi za kufanya maamuzi kwenye kanisa, ikiwemo kuwa mashemasi, na kwa waumini wa kawaida wa Kikatoliki kuwa na sauti zaidi ndani ya utawala wa kanisa. Wakati Papa Francis anaufungua mkutano huo wa kilele wa maaskofu, kundi dogo la waandamanaji limekusanyika katika Viwanja vya Mtakatifu Peter, mjini Vatican wakitetea hatua wa wanawake kuwekwa wakfu.

''Tumekusanyika hapa Roma kwenye ufunguzi wa Sinodi ya Maaskofu. Tuko hapa kuhakikisha kwamba sauti zote zinajumuishwa, miito yote inakaribishwa, na kura zote zinahesabiwa,'' alifafanua Kate McElwee, Mkurugenzi Mtendaji wa Kongamano la Kuwekwa Wakfu kwa Wanawake.

Wanawake walalamika kwa muda mrefu

Kwa muda mrefu wanawake wamelalamika kuwa wanachukuliwa kama raia wa daraja la pili katika kanisa, wamezuiwa kupata upadri na vyeo vya juu zaidi vya mamlaka, lakini wanawajibika kwa sehemu kubwa ya kazi ya kutoa mafundisho ya kanisa katika shule za Kikatoliki, kuendesha hospitali za Kikatoliki na kupitisha imani kwa vizazi vijavyo.

Papa Francis aliunda tume mbili za kufanya utafiti kuhusu suala hilo baada ya ombi kutolewa katika Sinodi iliyopita, lakini hadi sasa amekataa kufanya mabadiliko yoyote yale ndani ya kanisa.

Kumekuwepo pia na wito wa kutafuta njia bora za kuwakaribisha Wakatoliki wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, na wengine ambao wametengwa na kanisa, na hatua mpya za uwajibikaji katika kuangalia jinsi maaskofu wanavyotekeleza majukumu yao kuzuia unyanyasaji wa aina mbalimbali katika kanisa.

Kuna uwezekano Sinodi hiyo ya Maaskofu inayofanyika kuanzia Oktoba 4 hadi 28, ikaleta tena mgawanyiko mkubwa kati ya wapenda maendeleo na wahafidhina ndani ya Kanisa Katoliki lenye takribani waumini bilioni 1.4 ulimwenguni kote.

(AP, AFP)