1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiUlaya

Uingereza: Polisi 6,000 wako tayari kutuliza ghasia

6 Agosti 2024

Uingereza imesema maafisa maalumu 6,000 wa polisi wako tayari kukabiliana na vurugu zinazosababishwa na makundi ya mrengo mkali wa kulia ambazo zilizuka kufuatia mauaji ya watoto watatu na kuchochea mchafuko.

https://p.dw.com/p/4jBEW
Polisi Uingereza ikikabiliana na vurugu
Polisi Uingereza ikikabiliana na vurugu zinazosababishwa na makundi ya msimamo mkali.Picha: Hollie Adams/REUTERS

Waziri wa Sheria Heidi Alexander ameiambia redio ya BBC kuwa serikali imetengeneza nafasi 500 za ziada katika magereza ya nchi hiyo na imewaweka tayari polisi maalum 6,000 watakaokabiliana na vurugu.

Makundi ya watu yaliwashambulia polisi, wakachoma moto na kupora maduka huku wakiharibu vioo vya magari na majumba mwishoni mwa wiki. 

Aidha walizilenga hoteli mbili zinazowahifadhi waomba hifadhi katika miji kadhaa.

Soma pia:Starmer kuunda 'jeshi la dharura' kukabiliana na vurugu

Hapo jana, watu sita walikamatwa na polisi kadhaa wakajeruhiwa wakati waliposhambuliwa na wavusha vurugu waliokuwa wakiwarushia matofali na fataki katika eneo la Plymouth kusini mwa England.

Vurugu piazilishuhudiwa mjini Belfast, Ireland Kaskazini. Ghasia zilizuka mjini Southport Jumatano wiki iliyopita, siku moja baada ya wasichana watatu kuuawa na watoto wengine watano wakajeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu.

Uvumi wa uwongo awali ulisambazwa kwenye mitandao ya kijami ukisema kuwa mshambuliaji alikuwa muomba hifadhi wa kiislamu. Mshukiwa baadaye alitambuliwa kuwa Axel Rudakubana, mwenye umri wa miaka 17 mzaliwa wa Wales, na ambaye wazazi wake wanatokea Rwanda.