Polisi yapeleleza chanzo cha shambulizi la Prague
23 Desemba 2023Tukio hilo la Alhamisi katika Kitivo cha Sanaa cha Chuo Kikuu cha Charles ndilo shambulizi baya zaidi la aina hiyo kuwahi kufanywa katika Jamhuri ya Czech kwa miongo mingi.
Soma pia: Mwanafunzi awauwa takribani watu 14 kwa risasi Prague
Waombolezaji wameendelea kuwasha mamia ya mishumaa nje ya chuo hicho, huku taasisi hiyo, familia na marafiki wakianza kuchapisha majina ya waathirika. Mshukiwa wa shambulizi hilo, mwanafunzi wa umri wa miaka 24, alijiuwa baada ya kuwapiga risasi watu 13 na kuwajeruhi wengine 25.
Mmoja wa waliojeruhiwa alifariki baadae hospitalini. Lakini polisi imewakamata watu wanne ama kwa kutishia kuiga shambulizi hilo au kuliidhinisha. Serikali imetangaza siku ya maombolezi ya kitaifa leo Jumamosi, huku bendera kwenye majengo rasmi zikipepea nusu mlingoti na watu kuombwa kusalia kimya kwa dakika moja ifikapo saa sita kamili mchana.