1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAustralia

Polisi yasema shambulio la kisu Sydney lilikuwa la kigaidi

16 Aprili 2024

Polisi nchini Australia imesema shambulio la kisu mjini Sydney lililojeruhi askofu na kasisi na kuonekana moja kwa moja kwenye mtandao wa intanet wakati wa ibada ya kanisa kilikuwa kitendo cha ugaidi.

https://p.dw.com/p/4ep9J
Shambulio la kisu katika kanisa la Christ The Good Shephered
Karibu watu wanne walijeruhiwa katika tukio la kuchoma kisu ndani ya kanisa la Christ The Good ShepheredPicha: Paul Braven/AAP/REUTERS

Shambulio hilo lilifanywa wakati waumini waliojawa na hofu wakitizama mtandaoni na ana kwa ana. Polisi ilimkamata mvulana mwenye umri wa miaka 16 baada ya tukio hilo katika kanisa la Christ the Good Shephered ambalo lilimjeruhi Askofu Mar Mari Emmanuel na kasisi Isaac Royel. Wote wanaendelea kupata matibabu hospitalini na wako katika hali imara.

Soma pia: Polisi Australia yachunguza kwa nini muuwaji aliwalenga wanawake

Kamishna wa polisi wa New South Wales Karen Webb amesema matamshi ya mshukiwa huyo yaliashiria shambulio hilo kuchochewa na nia ya kidini. Kijana huyo alifahamika kwa polisi lakini hakuwa kwenye orodha ya wanaofuatiliwa kwa ugaidi.

Waumini walitizama wakati mtu aliyevalia nguo nyeusi alikaribia madhabahu na kumchoma kisu askofu huyo na kasisi wakati wa ibada ya kanisa jana jioni kabla ya wahudhuriaji kumzidi nguvu na kuwaita polisi. Umati wa mamia ya watu waliotaka kulipiza kisasi ulikusanyika nje ya Kanisa hilo la Orthodox, wakirusha matofali na chupa, na kuwajeruhi maafisa wa polisi na kuwazuia polisi kumtoa nje kijana huyo. Mshukiwa huyo na polisi wawili walilazwa hospitalini.