1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 18 wauawa na wanamgambo magharibi mwa Kongo

18 Septemba 2023

Maafisa wa serikali ya Kongo wamesema raia wapatao 18 na mwanajeshi mmoja wameuawa katika mashambulizi ya makundi ya wanamgambo magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4WSez
Wapiganaji wa Mobondo kusini magharibi mwa Kongo wanaendelea na mashambulizi dhidi ya raia
Wapiganaji wa Mobondo kusini magharibi mwa Kongo wanaendelea na mashambulizi dhidi ya raia Picha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamesema raia wapatao 18 na mwanajeshi mmoja wameuawa katika mashambulizi ya makundi ya wanamgambo magharibi mwa nchi hiyo, ambako ghasia baina ya makundi tofauti ya kijamii zimepamba moto tangu mwezi Juni mwaka jana (2022).

Wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri hapo jana, msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya, alisema raia hao inasadikika waliuawa Jumatatu iliyopita na wanamgambo wa "Mobondo" katika kijiji cha Final kilicho umbali wa kilomita 190 kusini mashariki mwa mji mkuu, Kinshasa.

Ghasia katika eneo hilo zilipungua katika miezi ya hivi karibuni kabla ya kupamba moto mwezi Machi, ambapo jamii ya Teke imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi kutoka kwa makundi ya watu wasio wakaazi halisi wa maeneo hayo yaliyo pembezoni mwa Mto Kongo.