Raia wa Moldova wapiga kura kuijiunga na Umoja wa Ulaya
21 Oktoba 2024Waungaji mkono wa Umoja wa Ulaya nchini Moldova, wamepata ushindi finyu katika kura ya nchi yao kuelekea kwenye Umoja huo. Baada ya asilimia 99.41ya kura milioni 1.4 kuhesabiwa, wanaounga mkono Moldova kujiunga na Umoja wa Ulaya walishinda kwa asilimia 50.39 na waliopinga walikuwa na asilimia 49.61.
Soma: Rais wa Moldova akosoa uvamizi dhidi ya demokrasia baada ya kura ya maoni
Matokeo hayo yamefahamika leo baada ya wananchi kushiriki katika kura ya maoni iliyokaribia kusababisha kipingamizi kikubwa kwa rais anayeunga mkono nchi za Magharibi ambaye ameyashutumu yale aliyoyaita "makundi ya wahalifu" kwa kujaribu kuhujumu zoezi la kupiga kura.
Kulingana na tume kuu ya uchaguzi wanaopinga kujiunga na Umoja wa Ulaya walikuwa wanaongoza hadi hivi karibuni. Rais wa Moldova Maia Sandu amesema pana ushahidi wa kuthibitisha kwamba wahalifu hao walikuwa na mpango wa kuzinunua kura 300,000 kwa kusaidiwa na mataifa ya nje.