Harakati ya 'Linda Niger' kuzinduliwa Jumamosi mjini Niamey
16 Agosti 2023Wakaazi katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wanawataka watu wajitolee na kujisajili kwa wingi ili kulisaidia jeshi kutokana na kuongezeka vitisho vya Jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ambayo imesema inaweza kutumia nguvu za kijeshi ikiwa jeshi la Niger halitamrejesha Rais Mohamed Bazoum waliyemuondoa madarakani mnamo tarehe 26 mwezi uliopita wa Julai.
Mwito huo, unaoongozwa na kundi la wenyeji wa mji mkuu wa Niger, Niamey, wanolenga kuwasajili maelfu ya watu kote nchini wanaotakiwa kujiandikisha kwa kujitolea kuilinda Niger.
Wanatakiwa watakaopigana, watakaosaidia kwenye huduma za matibabu za kiufundi na hata uhandisi vifaa miongoni mwa huduma zingine.
Amsarou Bako, mmoja wa waanzilishi, ameliambia shirika la Habari la Associated Press kwamba wanahitajika raia wenye uchungu na nchi yao kuwa tayari wakati wowote utakapotokea uvamizi. Harakati hiyo ya kuwasajili watu itazinduliwa siku ya Jumamosi katika mji wa Niamey vile vile katika miji ambayo inaweza kuvamiwa karibu na mipaka kati ya Niger na Nigeria na Benin, nchi mbili, ambazo zimesema zitashiriki iwapo ECOWAS itatoa agizo hilo.
Soma pia: Majenerali Niger wamrejesha nyumbani balozi wake kutoka Abidjan
Vyanzo vya kijeshi na vya kisiasa vimesema, wakuu wa kijeshi kutoka nchi za jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS watakutana nchini Ghana wiki hii kujadili uwezekano wa kuingilia kati nchini Niger.
Mkutano huo utakaofanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa ulipangwa kufanyika wikiendi iliyopita lakini ukaahirishwa na sasa utafanyika baada ya viongozi wa ECOWAS wiki iliyopita kuidhinisha kupelekwa kikosi cha uangalizi kwa ajili ya kurejesha utulivu wa kikatiba nchini Niger.
Wachambuzi wanasema uingiliaji kati wa kijeshi unaweza kuwa ni hatua ya hatari kiutendaji na pia hatari kisiasa, kwa kuzingatia mgawanyiko uliopo ndani ya safu za jumuiya ya ECOWAS na ukosoaji wa ndani ya nchi za kanda hiyo.
Wizara ya ulinzi ya Niger imesema kwenye taarifa yake kwamba wanajeshi 17 waliuawa katika shambulizi la kuvizia la hapo jana Jumanne katika eneo la kusini magharibi mwa Niger linalopakana na Burkina Faso.
Wakati hayo yakiendelea gharama za maisha zimezidi kupanda katika mji wa Niamey.
Wananchi wa Niger wanasema, wameanza kuhisi athari ya vikwazo vya usafiri na kiuchumi vilivyowekwa na jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS. Niger ina idadi ya watu milioni 25 na ni mojawapo kati ya nchi maskini zaidi duniani. Lakini licha ya kuwekewa vikwazo, viongozi wa kijeshi walioongoza mapinduzi wamekataa mapendekezo ya ECOWAS ya kumwachilia rais waliyemwondoa madarakani Mohamed Bazoum.
Soma pia: Utawala wa kijeshi wa Niger wasema upo tayari kwa mazungumzo
Mvutano kati ya Niger na jumuiya ya ECOWAS hauonyeshi dalili zozote za kupungua, licha ya ishara kutoka pande zote mbili kwamba wako tayari kuusuluhisha mgogoro huo kwa amani.
Wiki iliyopita jeshi lilisema liko tayari kufanya mazungumzo na ECOWAS lakini muda mfupi baadaye lilitangaza kuwa rais aliyeondolewa madarakani Bazoum atashtakiwa kwa makosa ya uhaini.