Raia watatu waliotekwa maandamano ya Gen-Z Kenya waachiliwa
20 Septemba 2024Mashirika ya haki za binadamu nchini humo yamevishutumu vikosi vya usalama kwa kutotoa taarifa ya eneo walikokuwa wameshikiliwa.
Watu hao, waliofahamika kama Bob Njagi, Aslam Longton na kaka yake Jamil Longton, wanadaiwa kutekwa mnamo Agosti 19 na wanaume waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi katika eneo la Kitengela, karibu kilomita 30 kusini mwa mji mkuu, Nairobi.
Soma zaidi: Ruto atetea rikodi ya uongozi wake wa miaka miwili
Hivi karibuni, tukio hilo lilipamba moto baada ya mahakama mjini Nairobi kumtia hatiani naibu mkuu wa jeshi la polisi, Gilbert Masengeli, kwa kosa la kudharau mahakama, kutokana na kushindwa kutokea mahakamani ili kujibu maswali juu ya kutoweka kwa watu hao watatu.
Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA) imesema inachunguza malalamiko kadhaa ya ukamataji wa kinyume cha sheria na utekaji kufuatia maandamano makubwa ya kuipinga serikali yaliozuka nchini Kenya mwezi Juni.