Rais Samia ampa Simba jina la Tundu Lissu
30 Agosti 2024Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa akitembelea maonesho ya kila mwaka katika visiwa vya nyumbani kwao Zanzibar siku ya Jumamosi alipowaona wanyama hao waliojawa na hasira kwenye banda la Wakala wa Taifa wa Wanyamapori.
Katika video iliyosambazwa sana mtandaoni, mlinzi anamwambia mnyama huyo alikuwa akienda kasi kwa sababu alikuwa bado hajala, kabla ya kusema paka huyo mkubwa hakuwa amepewa jina.
"Mpeni jina la mwanangu Tundu Lissu,” alipendekeza na kusababisha vicheko huku akioanisha jina lake maarufu la utani la "Mama Samia” na mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu.
Soma pia:Tundu Lissu akamatwa na polisi Arusha
Siku ya Jumapili, Samia alilinganisha tena "simba huyo mtundu na mkorofi" na Lissu "asiyetulia", ambaye aligombea urais mwaka 2020 kufuatia jaribio la mauaji mwaka 2017.
"Kwa hiyo, nilipendekeza apewe jina la Tundu Lissu kwa sababu ilikuwa na hekaheka kama za mwanagu Tundu Lissu.
Lissu apokea utani wa rais kwa bashasha
Lissu mwenye umri wa miaka 56 alikuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani waliokamatwa hivi karibuni katika jiji la kusini la Mbeya kabla ya kuadhimisha siku ya vijana.
Lakini Lissu, mkosoaji mkali wa chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi, aliuchukulia vyema utani wa rais.
"Rais Samia alikuwa sahihi kwani nilizaliwa katika familia ya mashujaa... watu walioua simba waliowashambulia ng'ombe," aliviambia vyombo vya habari vya ndani pia Jumapili.
Alieleza kuwa katika lugha ya Kibantu ya Kinyaturu, inayozungumzwa na kabila la Wanyaturu ambalo familia yake inatoka, watu hao walijulikana kama "ahomi" au "muhomi".
"Babu yangu mzaa baba Mughwai alikuwa muhomi. Aliua simba ambaye alishambulia na kuua ng'ombe wake," alisema na kuongeza kuwa babake pia "aliua simba mara mbili ambaye alishambulia na kuua ng'ombe wake".
Soma pia:Tundu Lissu na harakati za "mwanzo mpya" Tanzania
Mabadilishano hayo ya kirafiki yalikuja wiki chache tu baada ya polisi kuwaweka kizuizini viongozi wakuu wa chama cha upinzani nchini Tanzania - Chadema.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalilaani hatua hiyo, na kueleza wasiwasi kwamba hatua hiyo inaweza kuashiria kurejea kwa sera dhalimu za marehemu rais John Magufuli huku nchi ikijiandaa kwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao.
Samia aliingia madarakani mwaka 2021, kufuatia kifo cha Magufuli, na amepunguza vikwazo kwa vyombo vya habari na upinzani.