Rais wa Kongo aapishwa kwa muhula wa pili mbele ya kadamnasi
20 Januari 2024Huku hali ya wasiwasi ikitanda katika majimbo tete ya mashariki mwa taifa hilo, rais huyo mwenye umri wa miaka 60 anayejulikana kama "Fatshi" alichagua uwanja wa michezo wa Martyrs wa Kinshasa wenye uwezo wa kuchukua watu 80,000 kwa ajili ya sherehe hiyo.
Uwanja huo ulijaa kabla ya saa sita mchana huku wahudhuriaji wakiimba na kucheza dansi kwa wingi, huku karibu wakuu 20 wa mataifa ya Afrika walioalikwa wakihudhuria.
"Naapa kwa dhati...kutetea katiba na sheria za Jamhuri... kudumisha uhuru wake na mamlaka ya mipaka yake," rais huyo aliyechaguliwa tena alitangaza mbele ya majaji wa Mahakama ya Katiba, kabla ya kupokea salamu kutoka kwa machifu wa kimila wa mikoa 26 ya nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati.
"Ninafahamu matarajio yenu," Tshisekedi alitangaza baadae katika hotuba yake ya kuapishwa, akimaanisha miongoni mwa mambo mengine ukosefu wa ajira, vijana, wanawake na uwiano wa kitaifa.
Soma pia: Mahakama ya Katiba Kongo yaidhinisha ushindi wa Tshisekedi
Kuapishwa kwa Tshisekedi kwa mara ya kwanza, mnamo Januari 2019 baada ya kumshinda Martin Fayulu kwa utata, kulifanyika katika bustani ya Ikulu, katika ukumbi ambao kwa kawaida umekuwa ukiandaa matukio rasmi.
Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Kongo kushuhudia makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Safari ya kisiasa Tshisekedi
Tshisekedi ni mtoto wa marehemu kiongozi wa kihistoria wa upinzani Etienne Tshisekedi. Alichaguliwa rais kwa ahadi ya kuboresha hali ya maisha nchini DRC -- ambayo inajivunia utajiri wa madini lakini ina wakazi maskini zaidi ya milioni 100 -- na kukomesha miaka 25 ya umwagaji damu mashariki mwa nchi.
Hajatimiza ahadi hizo lakini safari hii alifanya kampeni kwa nguvu juu ya mafanikio yake ya muhula wa kwanza kama vile dawa za bure za msingi, akiomba mamlaka nyingine ya "kuimarisha" maendeleo.
Zaidi ya watu milioni 40 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzu wa Desemba 20 kuchagua rais, pamoja na wabunge wa kitaifa na wa mikoa na madiwani wa manispaa. Upigaji kura uliongezwa rasmi kwa siku ili kufidia ucheleweshaji mkubwa wa vifaa na kuendelea kwa siku kadhaa baadaye katika maeneo ya mbali.
Mwishowe, Tshisekedi alishinda rasmi kwa asilimia 73.47 ya kura. Moise Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga, aliibuka wa pili kwa asilimia 18.08. Martin Fayulu, ambaye anasema pia aliibiwa katika kura ya mwisho ya urais, alipata asilimia tano, huku mshindi wa tunzo ya amani ya Nobel Denis Mukwege akipata asilimia 0.22 pekee.
Soma pia: Baada kutangazwa mshindi, Tshisekedi anao mlima mrefu wa kupanda
Wagombea hawa walitaka matokeo ya uchaguzi yafutwe. Maandamano yaliyopangwa kufanyika Desemba 27 yalipigwa marufuku na kuzimwa na polisi. Askofu mkuu wa Kinshasa alishutumu uchaguzi huo na kuutaja kuwa ni vurumai kubwa na iliyopangwa.
Shutuma za udanganyifu na "ucheleweshaji wa uchaguzi" hazijapungua na hofu ya ghasia inasalia kuwa ya kweli katika nchi iliyo na historia ya machafuko ya kisiasa.
Wito wa maandamano ya wafuasi wa upinzani
Katumbi na Fayulu wametoa wito kwa wafuasi wao "kuonyesha kutoridhika kwao" siku ya Jumamosi. Waliwataka watu "kusimama na kusema 'hapana'", kutokea popote walipo, ingawa hakukuwa na dalili za maandamano katika mji mkuu, Kinshasa, siku ya Jumamosi.
Waandishi wa habari wa AFP walisema matairi ya gari yaliteketezwa Jumamosi asubuhi kwenye mitaa ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini lililokumbwa na vita.
Katika mji wa mkoa wa Beni, uliopo pia mashariki mwa Kongo, vijana walijaribu kuweka vizuizi lakini polisi waliingilia kati. Tume ya uchaguzi CENI imetambua visa vya udanganyifui, uharibifu na vitisho, pamoja na matumizi ya mashine haramu za kupigia kura.
Katika uchaguzi mkuu, kura zimebatilishwa kwa wagombea 82 -- wakiwemo mawaziri watatu wa serikali na magavana wanne wa majimbo. Changamoto ya usalama inasalia kuwa kubwa kwa Tshisekedi.
Soma pia: Upinzani Kongo wagoma kuwasilisha pingamizi mahakamani
Kulikuwa na utulivu katika mapigano mashariki wakati wa uchaguzi lakini ghasia zimeanza tena kati ya jeshi na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda.
Tangu katikati ya mwezi Desemba, wanajeshi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) yenye mataifa 10 wamekuwa wakiwasili DRC kwa siri.
Wanachukua jukumu kutoka kwa kikosi cha kulinda amani cha Afrika Mashariki ambacho muda wake ulikatizwa na serikali ya DRC, ikikishtumu kushirikiana na waasi badala ya kupigana nao.
Afisa mkuu wa jeshi alisema Jumanne kwamba Kinshasa inawategemea kusaidia kurejesha maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23, ambao wameteka maeneo mengi ya mashariki tangu kuanzisha tena vita mwaka 2021.