Emmanuel Macron katika ziara ya siku tatu barani Afrika
26 Julai 2022Serikali ya Cameroon iliupamba mji wake mkuu ili kumpokea rais Macron. Tingatinga zilibomoa vibanda katika masoko na mitaa ya Yaounde, kulikopita msafara wa Macron. Solange Kemje, mwenye umri wa miaka 28, miongoni mwa mamia ya wamiliki wa vibanda walioathirika, amesema wameharibu chanzo chake pekee cha kujikwamua maishani.
Watu wengine wameipokea vyema ziara ya kiongozi huyo wa Ufaransa, wakitumai kwamba Macron ataongeza msaada katika kukabiliana na ongezeko la ukosefu wa usalama unaosababishwa na makundi ya kigaidi yaliyotokea nchi jirani ya Nigeria.
Taifa hilo la Afrika ya kati linapambana pia na mzozo wa wa wanaotaka kujitenga, mzozo ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, umesababisha vifo vya watu wasiopungua 3,300 na kupelekea wengine zaidi ya 750,000 kuyahama makazi yao katika kipindi cha miaka mitano.
Soma zaidi:Vita vya Cameroon vilivyosahaulika vyawaacha wakimbizi njiapanda
Makundi ya waasi yanapigania jamii ya walio wachache nchini Cameroon na wanaozungumza lugha ya Kiingereza, kuweza kuwa na nchi yao iliyo huru na itakayoitwa Ambazonia. Makundi hayo wanatumai kuwa Macron atamshawishi Rais Paul Biya kukomesha matumizi ya nguvu kama suluhisho la mzozo huo.
Lakini serikali ya Cameroon inasema Ufaransa inaunga mkono jeshi lake kupambana na watu wanaotaka kujitenga pamoja na ghasia za kigaidi kutoka kwa waasi wa Boko Haram wa Nigeria lakini haikufafanua kiwango cha silaha ilizopokea kutoka kwa Ufaransa.
Macron kumshawishi Paul Biya kustaafu?
Baadhi ya watu wanatumai kuwa Macron atamshawishi Paul Biya rais wa Cameroon mwenye umri wa miaka 89 na ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miaka 40, kufikia uamuzi wa kustaafu. Biya anatuhumiwa kwa udanganyifu wa uchaguzi ili kusalia madarakani hadi kifo chake, lakini amekuwa akikana tuhuma hizo na kusema alishinda uchaguzi kwa njia ya haki na ya kidemokrasia.
Mwanasiasa Prince Ekosso amesema ushawishi wa Ufaransa umepungua nchini Cameroon baada ya nchi hiyo kusaini mkataba wa ulinzi na Urusi na kutoa ruhsa ya uchimbaji madini kwa China. Baadhi ya wadau wanatarajia kumuomba Macron afikiriye upya vikwazo vya kibiashara vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi.
Soma zaidi:Macron aandaa mkutano wa kilele kuhusu Afrika
Macron hata hivyo amesema, bara la Afrika linatakiwa kuzalisha zaidi ili kujitegemea:
"Ni wazi kwamba tunashambuliwa na baadhi ya watu wanaolaumu vikwazo vya Ulaya kuwa chanzo cha mzozo wa chakula duniani na Afrika. Ni upuuzi na uwongo. Chakula na nishati vimekuwa silaha za kivita vya Urusi. Lazima tulisaidie bara la Afrika kujitosheleza zaidi na mazao yake yenyewe."
Katika ziara hiyo Macron ameandamana wakuu wa maswala ya kigeni, kijeshi na maendeleo na atajaribu kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kukomesha kuenea kwa ugaidi kote Afrika Magharibi ikiwa ni pamoja na Cameroon, Benin na Togo. Baada ya Cameroon, Macron ataelekea Benin na Guinea Bissau.
(APE)