Rais wa Uzbekistan ashinda muhula mwingine madarakani
10 Julai 2023Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev ameshinda muhula wa tatu madarakani baada ya uchaguzi uliofanyika jana, matokeo yanayomwezesha kuendelea kuitawala nchi hiyo ya Asia ya Kati yenye utajiri mkubwa wa mafuta hadi mwaka 2030.
Matokeo ya awali yanaonesha Mirziyoyev aliyekuwa akichuana na wagombea wengine watatu wasio na umaarufu mkubwa amepata ushindi wa asimilia 87 ya kura.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 65 aliahidi mageuzi makubwa wakati wa kampeni ikiwemo kukaribisha uwekezaji wa kigeni na kuifufua sekta ya utalii ya taifa hilo lililokuwa sehemu ya Dola ya Kisovieti.
Soma pia: Uzebkistan yaidhinisha mabadiliko yatakayorefusha utawala wa rais
Rais Xi Jinping wa China na Vlamidir Putin wa Urusi wamekuwa viongozi wa kwanza wa ulimwengu kutuma salamu za pongezi kwa Mirziyoyev ambaye anaiongoza Uzbekistan tangu mwaka 2016.
Ushindi wake unafuatia mabadiliko ya katiba yaliyofanyika mwaka huu yaliyomruhusu kuwania tena kiti cha urais kwa mihula mingine miwili ya miaka saba.